MAREKANi-SIASA-UCHUMI

Shughuli za serikali zaendelea kukwama Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump katika ikulu ya White House Washington Januari 2.
Rais wa Marekani Donald Trump katika ikulu ya White House Washington Januari 2. REUTERS/Jim Young

Siku ya 12 ya "mvutano" nchini Marekani kufuatia kukwama kwa shughuli za serikali, mazungumzo kati ya Rais Donald Trump na wakuu wa vyama bungeni, yameambulia patupu mjini Washington.

Matangazo ya kibiashara

Donald Trump ameonyesha umuhimu wa ukuta anaotaka kujenga kwenye mpaka na Mexico, Lakini wapinzani wake wa Democrats wamekataa katu katu kufadhili mradi huo.

"Hali hii Inaweza kudumu kwa muda mrefu," amesema rais wa Marekani, ambaye amewatolewa wito viongozi kutoka pande zote mbili kukutana tena Ijumaa.

Huenda mambo yakachukua sura mpya leo Alhamisi, pale wajumbe wa Baraza la Wawakilishi watakapofanya kikao cha kwanza mwaka 2019, chini ya udhibiti wa chama cha Democratic.

Rais Trump amesema atakaidi kuitia saini bajeti yoyote hadi pale matakwa yake ya dola bilioni 5 za kujenga ukuta kwenye mpaka na Mexico yatakaporidhiwa, na mtu anayetarajiwa kuchaguliwa baadaye leo kuwa spika wa baraza la wawakilishi, Nancy Pelosi, amesema hata ikichukua muda gani, hawatakubali masharti hayo ya Trump.

"Haijalishi muda itakaochukuwa, wala mara watakazoulizwa, jibu litabakia kuwa hapana kwa ujenzi wa ukuta, " Bi Pelosi amesema katika mahojiano na shirika la habari la NBC la nchini Marekani.

Kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico ilikuwa ahadi muhimu ya kampeni ya Rais Trump, na kulingana na afisa mmoja wa Ikulu ya White House aliyenukuliwa na shirika la habari la Associted Press, amethibitisha kuwa Trump katika kikao na viongozi wa vyama, alitamka kwamba hawezi kuachana na azma ya kuujenga ukuta huo, kwa sababu akifanya hivyo ataonekana mjinga.