VENEZUELA-SIASA

Venezuela: Guaido atoa wito wa kufanyika maandamano kushinikiza jeshi

Juan Guaido kiongozi mkuu wa upinzani amtia tumbo joto rais wa Venezuela Nicolas Maduro.
Juan Guaido kiongozi mkuu wa upinzani amtia tumbo joto rais wa Venezuela Nicolas Maduro. France24

Juan Guaido, aliyejitangaza rais wa mpito wa Venezuela ametoa wito wa kufanyika kwa maandamano mapya Jumatano na Jumamosi kwa lengo la kushinikiza jeshi, linaloendelea kumtii Rais rais aliyechaguliwa Nicolas Maduro, na kuunga mkono onyo la Ulaya kwa ajili ya uchaguzi huru.

Matangazo ya kibiashara

"Jumatano kuanzia saa sita hadi saa nane mchana, nchini kote Venezuela tutamiminika mitaani (...) kuomba jeshi la nchi kuunga mkono madai ya wananachi, na Jumamosi (tunatoa wito) wa kufayika kwa maandamano kubwa nchini Venezuela na kwingineko duniani kuunga mkono onyo la Umoja wa Ulaya, "amesema Juan Guaido, Spika wa bunge la venezuela, mwenye umri wa miaka 35.

Siku ya Jumamosi nchi sita za Ulaya (Uhispania, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Ureno, Uholanzi) zilimpa Nicolas Maduro muda wa siku nane kuitisha uchaguzi, la sivyo zitamtambua Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela. Muda huo utatamatika siku ya Jumapili.

Tayari Marekani na nchi kadhaa za Amerika Kusini zimetangaza kuwa zinamtambuwa Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela.

Kwa upande wa kimataifa, nchi ndogo zinamuunga mkono Nicolas maduro, ikiwa ni pamoja na China, Uturuki, Mexico na Urusi.

hata hivyo Juan Guaido ameendelea kupokea uungwaji mkono.

Siku ya Alhamisi jioni alitangaza kwamba anataka kuandaa haraka uchaguzi mpya.

Hivi karibuni Waziri wa Ulinzi, Jenerali Vladimir Padrino, alionekana katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi wiki hii huko Caracas akizungukwa na uongozi wa jeshi katika ngazi ya juu ili kulaani "jaribio la mapinduzi" lililofanywa na spika wa Bunge.

"Ninatoa tahadhari kwa raia wa Venezuela kwamba jaribio la mapinduzi limefanywa dhidi ya taasisi za uongozi wa nchi, dhidi ya demokrasia, dhidi ya Katiba yetu, dhidi ya Rais Nicolas Maduro, rais wetu halali," alisema waziri huyo.

Awali Majenerali wanane ambao wanaongoza Majimbo muhimu ya nchi hiyo walisema bado "wanamtii" Rais Nicolas Maduro, katika ujumbe uliorushwa kwenye televisheni ya serikali.