VENEZUELA- EU-MAANDAMANO-SIASA

Guaido apata uungwaji mkono kutoka bunge la Ulaya

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani anayemtia tumbo joto rais Nicolas Maduro.
Juan Guaido, kiongozi wa upinzani anayemtia tumbo joto rais Nicolas Maduro. France24

Bunge la Ulaya limetangaza kwamba linamtambua kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido kama "rais halali wa mpito" nchini humo. Katika azimio lililopitishwa Brussels, wabunge wa Umoja wa Ulaya wametoa wito kwa nchi zote wanachama wa umoja huo kumtambua Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huo huo Juan Guaido anasema amefanya mazungumzo ya siri na wanajeshi kutafuta uungwaji mkono wao wa kumng'atua madarakani rais Nicolás Maduro.

"Tumefanya mkutano wa dharura na vikosi vya usalama," amesema Bw. Guaido.

"Majeshi kuondoa msaada wao kwa Nicolas Maduro ni sehemu muhimu sana katika harakati ya kuleta mageuzi serikalini. Watu wengi wanaamini kuwa suluhisho la mzozo unaokumba nchi hii hauwezi kokomeshwa chini ya utawala huu," ameongeza Juan Guaido

Mwezi uliyopita Bw. Guaido alijitangaza kuwa rais wa mpito katika hatua ambayo imeungwa mkono na Marekani na mataifa kadhaa ya Amerika kusi pamoja na nchi kadhaa za Ulaya.

Hayo yanajiri wakati Mahakama ya juu zaidi chini Venezuela imemwekea marufuku kiongozi wa upinzani kutoondoka nchini na pia kupiga tanchi akaunti zake za benki.