VENEZUELA- EU-MAANDAMANO-SIASA

Nchi 19 za Ulaya zamtambua Juan Guaido kama rais wa Venezuela

Juan Guaidó Aliyejitangaza rais wa mpito Venezuela.
Juan Guaidó Aliyejitangaza rais wa mpito Venezuela. REUTERS/Carlos Garcia Rawlins

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaido ametambuliwa kama rais wa mpito wa Venezuela na nchi 19 za Umoja wa Ulaya, mara baada ya kushtumiwa na Nicolas Maduro "kuunga mkono mpango wa jaribio la mapinduzi" wa Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Wakati Juan Guaido, 35, akiendelea kupata uungwaji mkono, amesema anajaribu kukusanya misaada ya kibinadamu kuifikisha nchini Venezuela, ambapo raia wanakabiliwa na uhaba mkubwa.

Siku ya Jumatatu, siku moja baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho uliyotolewa na nchi kadhaa za Ulaya ambazo zilimtaka rais Nicolas Maduro kuitisha uchaguzi mpya wa urais, nchi 19 za Umoja huo ikiwa ni pamoja na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamechukua hatua na kumtambua Bw Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela.

Uungwaji huu mkono, ulioshtumiwa na Urusi, moja wa washirika wakuu wa Maduro kwamba ni "kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela", unakuja baada ya Marekani, Canada na nchi kumi na mbili za Amerika Kusini ikiwa ni pamoja na Colombia. na Brazil kuonyesha msimamo wao dhidi ya Nicolas Maduro.

Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umegawanyika: Italia imezuia taarifa ya pamoja ya Umoj umoja huo, kulingana na vyanzo vya kidiplomasia kutoka Brussels.

Serikali ya Venezuela imetangaza kuwa "itapitia upya" mahusiano yake ya kidiplomasia na nchi za Ulaya ambazo zimemtambua Juan Guaido kama rais wa mpito Venezuela, ikishtumu kuunga mkono "mpango wa jaribio la mapinduzi" wa Marekani".

Marekani imekaribisha hatua ya nchi hizo za Umoja wa Ulaya kumtambua Juan Guaido kama rais wa mpito wa Venezuela na kutolea wito nchi nyingne kufanya hivyo.