VENEZUELA-IFRC-SIASA-UCHUMI

Maduro akubali kupokea msaada wa kibinadamu kutoka shirika la Msalaba Mwekundu

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro. Miraflores Palace/via REUTERS

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro ametangaza kwamba Venezuela imefikia "makubaliano" na Shirikisho la Kimataifa la mashirika ya Msalaba Mwekundu (IFRC) ili kutoa msaada wa kibinadamu.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa Mambo ya Nje, Jorge Arreaza, anafanya mazungumzo na IFRC kuhusu"waraka rasmi," amesema Nicolas Maduro, ambaye awali alikataa kwamba hakuna mgogoro wa kibinadamu katika nchi yake.

Mwezi Februari mwaka huu kiongozi huyo wa kisoshalisti alikataa kuruhusu msaada wa kibinadamu, akisema anahofia kwamba magari ambayo yangelileta msaada huo yangelitumiwa kwa kuwezesha watu wenye silaha kutoka nchi za kigeni kuingia nchini Venezuela na kuhatarisha usalama wa taifa.

Tangazo hilo linakuja siku ambapo kunatarajia kufanyika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulioombwa na Marekani ili kujadili mgogoro wa kibinadamu nchini Venezuela.

"Mahitaji ya msaada ni muhimu," Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Mambo ya Kibinadamu na Mratibu wa Usaidizi wa Dharura, Mark Lowcock, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Tunaweza kufanya zaidi ili kupunguza mateso ya wananchi wa Venezuela, ikiwa tunaweza kuwa na msaada zaidi na uungwaji mkono kutoka kwa wadau wote," ameongeza.

Wakati huo huo Makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence, ameomba kwa mara nyingine Umoja wa Mataifa kumtambua kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido kama rais halali.

"Muda umewadia kwa Umoja wa Mataifa kumtambua rais wa mpito Juan Guaido kama rais halali wa Venezuela na tunaomba wakubali kuweka wawakilishi wake" katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, amesema Mike Pence mbele ya taasisi hiyo ya kimataifa.

Ameongeza kuwa Marekani itawasilisha rasimu ya azimio kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rasimu ya azimio la awali lililoandaliwa na Marekani lilizuiwa na Urusi na China, washirika wakuu wa Nicolas Maduro, ambao walitumia kura yao ya veto.