MAREKANI-YEMEN-USALAMA

Trump atumia kura yake ya veto kwa kuzuia azimio la Baraza la Congress kuhusu Yemen

Rais wa Marekani Donald Trump ndani ya ikulu ya ikulu ya White House, Aprili 12, 2019.
Rais wa Marekani Donald Trump ndani ya ikulu ya ikulu ya White House, Aprili 12, 2019. NICHOLAS KAMM / AFP

Rais wa Marekani Donald Trump ametumia kura yake ya veto kama rais, kuzuia azimio lililopitishwa mapema mwezi huu na Baraza la Congress la Marekani, linaloomba Marekani kuacha kusaidia muungano unaongozwa na Saudi Arabia katika vita nchini Yemen, ikulu ya White House imetangaza.

Matangazo ya kibiashara

"Azimio hili ni jaribio lisilofaa na ni hatari kwa kudhoofisha mamlaka yangu ninayoruhusiwa na Katiba. Azimio ambalo linahatarisha maisha ya raia wa Marekani na wanajeshi, leo na katika siku zijazo," amesema Donald Trump katika ujumbe uliotumwa na ikulu ya White House.

Wabunge kadhaa kutoka chama cha Republican walijiunga na wale wa chama cha Democratic kwa kupigia kura azimio linaloomba jeshi la Marekani kuacha kushiriki katika vita nchini Yemen - ikiwa ni pamoja na msaada unaotolewa kwa muungano huo unaoongozwa na Saudi Arabia kwa mashambulizi ya angani- mpaka lipate idhini kutoka Baraza la Congeress.

Muswada wa azimio hilo ulipitishwa katika Bunge la Seneti mnamo mwezi Machi, ambapo Chama cha Republican kina idadi kubwa ya wajumbe, kabla ya kupitishwa mwezi huu katika Baraza la Wawakilishi, lenye wabunge wengi kutoka chama cha Democratic.

Ikulu ya White House ilionya kwamba Donald Trump atatumia kura yake ya veto kama rais ikiwa azimio hilo litapitishwa na Baraza la Congress.

Kwa kupinga kura hii ya veto, Bunge la Seneti na Baraza la Congress wanatakiwa kupiga kura na kupitisha muswada huo wa azimio kwa theluthi mbili sawa na kura zaidi ya zile zilizopigwa awali.