VENEZUELA-MADURO-SIASA-USALAMA

Kiongozi wa upinzani Venezuela atoa wito kwa wananchi kususia shughuli za serikali

Makabiliano makali kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji yazuka karibu na kambi ya jeshi la anga ya La Carlota, mashariki mwa Caracas, Mei 1, 2019.
Makabiliano makali kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji yazuka karibu na kambi ya jeshi la anga ya La Carlota, mashariki mwa Caracas, Mei 1, 2019. Federico PARRA / AFP

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Juan Guaidó ametaka kufanyika kwa migomo nchini humo kuendeleza shinikizo za kuondoka madarakani kwa rais Nicolás Maduro.

Matangazo ya kibiashara

Guaido amewaambia wafanyakazi wa Serikali kutoenda kazini leo Alhamisi na badala yake kuungana na waandamanaji wa upinzani.

Polisi na waandamanaji wameendelea kukabiliana jijini Caracas na jana mwanamke mmoja aliuawa katika makabiliano hayo.

Marekani inaongoza shinikizo za kuondoka madarakani kwa rais Maduro.

serikali ya Marekani imesema inafuatilia kwa uangalifu hali inayoendelea nchini Venezuela. Marekani inaendelea kushinikiza Nicolas Maduro kuondoka nchini.

Siku nzima ya Jumanne, viongozi wa Marekani waliendelea kuongeza shinikizo kwa utawala wa Maduro na nchi zinazomuunga mkono. Makamu wa rais Mike Pence na Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo, kwenye Twitter, walikuwa wakikaribisha operesheni ya "kujikomboa" iliyozinduliwa na Juan Guaido na kuthibitisha uungwaji wao mkono kwa mabadiliko ya amani kuelekea demokrasia.

John Bolton, kwa upande wake, amekumbusha kwamba mambo yote yanajadiliwa kuung'oa utawala wa Maduro, huku akimuonya Maduro kutotumia nguvu dhidi ya raia.