VENEZUELA-MADURO-SIASA-USALAMA

Maduro atoa wito kwa jeshi kutowatega sikio maadui wa Venezuela

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro ametoa wito kwa wanajeshi wa nchi hiyo kuwapinga watu wanaotaka kufanya mapinduzi, siku chache tu baada ya sehemu ya wanajeshi kujitokeza kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Juan Guaido.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika mkutano na maafisa wa jeshi, Caracas.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro katika mkutano na maafisa wa jeshi, Caracas. REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Rais Maduro ametoa kauli hii wakati alipokutana na mamia ya wanajeshi wa nchi hiyo mjini Caracas na kuwataka kusimama kidete kutetea nchi yao dhidi ya aliowaita wasaliti na wachochezi.

Jumanne ya wiki hii kinara wa upinzania Juan Guaido ambaye anatambuliwa na zaidi ya mataifa 50 kama rais wa mpito wa Venezuela, alitoa wito kwa wanajeshi kumtenga Maduro na kuungana na kambi yake.

Kwa wanajeshi kuendelea kumuunga mkono rais Maduro kuna maanisha kuwa bado Guaido hajapata uungwaji mkono wa kutosha kutoka kwa jeshi, jeshi ambalo linatuhumiwa kwa vitendo vya rushwa na kuungwa mkono na Urusi.

Leo Ijumaa kunatarajiwa maandamano makubwa katika mji mkuu Caracas.