MAREKANI-CHINA

Huawei: Mabilioni ya wateja kuathirika na hatua ya Marekani

Mwanasheria wa kampuni ya mawasiliano ya China ya Huawei, amesema uamuzi wa Marekani kuiorodhesha katika makampuni yanayolengwa kibiashara itaathiri mabilioni ya watumiaji wake.

Nembo ya kampuni ya Huawei
Nembo ya kampuni ya Huawei 路透社
Matangazo ya kibiashara

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Song Liuping amesema katazo la kibiashara la Marekani pia litawaathiri moja kwa moja makampuni ya Kimarekani pamoja na ajira.

Hivi karibuni utawala wa Washington uliiorodhesha Huawei katika msururu wa makampuni ambayo Marekani imeyapiga marufuku kufanya nao biashara labda tu wapate leseni maalumu.

Makataa haya ya kibiashara ni sehemu ya vita ya kibiashara baina ya mataifa hayo mawili yenye nguvu duniani..

Marekani ilichukua uamuzi wa kuizuia Huawei ambayo ni wazalishaji wakubwa duniani wa vifaa vya mawasiliano kwa kile ilichodai kuwa kampuni hiyo imekuwa ikidukua taarifa na ni hatari kwa usalama.

Huawei mara zote imekuwa ikikanusha tuhuma za Marekani ikisisitiza kuwa ni kampuni huru na haina uhusiano wowote na Serikali.

Huawei sasa inasema uamuzi wa Marekani kuiorodhesha kampuni yao kama moja ya makampuni mabaya kiusalama, inamadhara makubwa kuliko utawala wa Washington unavyokadiria.

"Uamuzi huu unatishia kuwadhuru zaidi ya wateja wetu katika nchi 170 duniani, wakiwemo watu bilioni tatu ambao wanatumia bidhaa na huduma za Huawei," imesema taarifa ya kampuni hiyo.

Taarifa ya Huawei imeongeza kuwa "Kwa kuzuia makampuni ya kimarekani kufanya biashara na Huawei, Serikali itaathiri makampuni elfu 1 na 200 na ajira za mamilioni ya wamerekani zitakuwa mashakani."