MAREKANI

Rais Donald Trump agadhabishwa na matamshi ya Mueller

Rais wa Marekani, Donald Trump
Rais wa Marekani, Donald Trump MANDEL NGAN / AFP

Rais wa Marekani, Donald Trump amekosoa vikali matamshi ya aliyekuwa kiongozi wa jopo la uchunguzi ikiwa Urusi iliingilia uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza kwa mara ya kwanza Jumatano ya wiki hii, Mueller aliweka wazi kuwa uchunguzi wake ulibaini uwepo wa makosa yaliyofanywa na rais Trump kutaka kukwepa sheria, lakini akashindwa kufikia hitimisho kutokana na sheria iliyopo kwenye wizara ya sheria.

Matamshi ya Mueller yalikuwa kama msumari wa moto katika tuhuma zinazomkabili rais Trump ambaye ameendelea kupambana kusafisha jina lake kutokana na tuhuma za kusaidiwa na Urusi kushinda uchaguzi mkuu uliopita.

Sasa rais Trump anasema anashangazwa na matamshi ya Mueller ambaye hajawahi kumpenda katika historia ya uhusiano wao na kuongeza kuwa alikuwa wa kwanza kupinga uteuzi wake kuongoza jopo kumchunguza.

Rais Trump pia amewakosoa wabunge wa Democrats ambao amesema wanatafuta mchawi bila mafanikio, akiwaita ni watu wanaotafuta umaarufu kupitia utawala wake.

Saa chache baada ya aliyekuwa kiongozi wa timu ya wachunguzi kuhusu ikiwa Urusi iliingilia uchaguzi mkuu wa Marekani kufafanua kile kilichomo kwenye ripoti yake, wanasiasa watatu wa juu wa chama Democrats wametoa wito wa kuanzishwa mchakato wa kumuondoa madarakani rais Donald Trump.

Akizungumza kwa mara ya kwanza Jumatano ya wiki hii, Robert Mueller amesema uchunguzi walioufanya haukumfutia hatia rais Trump ya kukiuka sheria, akitofautiana pakubwa na matamshi ya Trump.

Mueller alikuwa amepewa jukumu la kuchunguza ikiwa Urusi iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016.

Kwenye hotuba yake, Mueller amesema suala la kumfungulia mashtaka rais aliyeko madarakani halikuwa ni suala lililoko mezani kwa wakati ule.

Suala la mchakato wa kumuondoa Trump madarakani limewagawa wabunge wa chama cha Democrats, ambapo baadhi wamejitokeza kuongeza shinikizo kwa spika wa bunge Nancy Pelosi, ambaye mpaka sasa hajakubali kuanzisha mchakato huo.

Matamshi ya Mueller sasa yamewaibua wagombea wengine watatu wanaoomba kuchaguliwa na chama chao kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, wakifanya idadi yao kuwa 10 ya wanaotaka mchakato wa kumuondoa Trump uanze.

Rais Trump kwa upande wake ameendelea kusisitiza kutokuwa na hatia akisema sheria zilizopo haziruhusu rais aliyeko madarakani kushtakiwa na hivyo mjadala wa Mueller umefungwa rasmi.