MAREKANI-MEXICO

Rais Trump atangaza tozo kwa bidhaa za Mexico kukabiliana na wahamiaji

Rais wa Marekani, Donald Trump akizungumza nje ya ikulu ya Washington. Tarehe 30/05/2019
Rais wa Marekani, Donald Trump akizungumza nje ya ikulu ya Washington. Tarehe 30/05/2019 REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani, Donald Trump juma hili amesema nchi yake itatangaza tozo ya asilimia 5 kwa bidhaa kutoka nchini Mexico, ikiwa ni hatua aliyosema inalenga kuishinikiza nchi hiyo kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaoingia nchini mwake.

Matangazo ya kibiashara

Rais Trump amesema tozo hizi zitaanza Juni 10 na kisha zitaendelea kuongezeka kwa awamu hadi kufikia asilimia 25 ifikapo Octoba Mosi mwaka huu na kwamba zitasalia kwa kiwango hicho hadi pale Mexico itakapozuia wahamiaji wanaopitia kwenye mpaka wake.

"Kama mnavyojua, Marekani imekuwa ikivamiwa na mamia ya wahamiaji kutokea Mexico na kuingia nchini mwetu kinyume cha sheria. Wimbi la wahamiaji limekuwa na madhara makubwa kwa nchi yetu na maisha ya watu," ilisema taaifa ya rais Trump.

Rais Trump kwenye taarifa yake amesema ikiwa Mexico itachukua hatua kali kudhibiti wimbi la wahamiaji wanaoingia nchini mwake, basi tozo hizo zitaondolewa.

Nchi ya Mexico ni taifa latatu linalofanya biashara na Marekani kwenye maeneo ya mpaka. Marekani iliagiza bidhaa zinazofikia thamani ya dola bilioni 346.5 mwaka uliopita, huku nusu kati ya hizo zilikuwa ni magari na mashine/

Marekani kwa upande wake inasafirisha biadhaa zinazofikia thamani ya dola bilioni 265 kwendas Mexico.