MAREKANI-SIASA-USALAMA

"Maadui wa Marekani": Trump atetea mashambulizi yake dhidi ya wabunge

Rais wa Marekani Donald Trump, Washington, Julai 15, 2019.
Rais wa Marekani Donald Trump, Washington, Julai 15, 2019. REUTERS/Kevin Lamarque

Baada ya kuomba wabunge kutoka chama cha Democratic kurudi katika nchi ambazo walitoka, rais wa Marekani Donald Trump amebaini kwamba wabunge hao ndio wanatakiwa kuomba radhi, hapana yeye.

Matangazo ya kibiashara

Donald Trump ameendelea kutoa matamshi yake makali dhidi ya wabunge kutoka chama cha Democratic. Baada ya kuandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter, akiwataka wabunge wanne kutoka chama cha Democratic "kurudi katika nchi walikotoka", rais Donald Trump amerejelea kauli yake hiyo na kuwataka wabunge hao kuomba radhi kwa wananchi wa Marekani. Akitaja hatua zao kama za "kutisha", huku akiwashtumu kwamba wanapenda "maadui wa Marekani".

Donald Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba ujumbe wake hauhusiani na ubaguzi wowote, huku akibaini kwamba watu wengi walikubaliana naye na kwamba kama mtu hataki kuishi katika nchi hiyo (Marekani), analazimika kuondoka.

Hata kama hakutaja majina yao, kila mtu anajua kwamba rais wa Marekani alimaanisha wabunge Alexandria Ocasio-Cortez, Ilhan Omar, Rashida Tlaib na Ayanna Pressley, ambao mara kwa mara hupiga picha pamoja, na kuziweka hasa kwenye mitandao ya kijamii. Mbali na Ilhan Omar, mkimbizi kutoka Somalia, ambaye aliwasili nchini Marekani akiwa mtoto Marekani, wengine watatu wanaosalia walizaliwa nchini Marekani.

Baada ya ujumbe huo wabunge hao hawakuchelewa kujibu. Aleksandria Ocasio-Cortez, mzaliwa wa Puerto Rico na maarufu sana katika chama cha democratic, amemshtumu rais wa Marekani kwa kutumia lugha chafu ya kibaguzi.

Wakizungumza na waandishi wa habari wanawake hao wamesema, hivi sasa watu waweke akili zao kwenye sera za nchini Marekani na si maneno ya rais Donald Trump.

Kwa pamoja bi Omar na bi Tlaib wamerejea wito wa kutaka bw Trump apigiwe kura ya kutokuwa na imani naye.

Katika taarifa, Seneta kutoka chama cha Republican Susan Collins pia amelaani maneno "yasiyofaa" na akasema ujumbe wa rais unapaswa "kuondolewa haraka" kwenye ukurasa wake wa Twitter.