MAREKANI-SIASA-USALAMA

Donald Trump atangaza kujiuzulu kwa mkuu wa ujasusi mwezi ujao

Mara kadhaa, mkuu wa ujasusi Dan Coats altofautiana kwa maoni na rais Trump.
Mara kadhaa, mkuu wa ujasusi Dan Coats altofautiana kwa maoni na rais Trump. NICHOLAS KAMM / AFP

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba Mkuu wa ujasusi wa Marekani, Dan Coats, ataachia wadhifa wake mwezi ujao wa Agosti.

Matangazo ya kibiashara

Trump ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa Coats ataondoka Agosti 15, akisema mipango imekamilika ya kumteuwa Mbunge John Ratcliffe wa Texas, ambaye ni mwanachama wa kamati za bunge kuhusu ujasusi, mahakama na usalama wa ndani, kuchukua nafasi hiyo.

Kuondoka kwa Coats, ambaye hata hivyo aliepuka sana mabishano ya moja kwa moja na Trump - ni tukio la karibuni la afisa wa ngazi ya juu kujiuzulu katika utawala mgumu wa rais huyo.

Wawili hao walitofautiana katika masuala mbalimbali. Dan Coats wakati mwingine hakuweza kuficha tofauti zake na rais wa Marekani. Hivi karibuni aliunga mkono ripoti ya ujasusi inayothibitisha kwamba Urusi iliingilia uchaguzi wa rais wa Marekani wa 2016 ambao ulimuweka Trump madarakani.

Mkuu wa ujasusi pia alipinga hadharani uamuzi wa rais Donald Trump kuwa alifanya mazungumzo ya faragha na rais wa Urusi Vladimir Putin huko Helsinki katika majira ya joto mwaka jana, huku wakiwepo wakalimani pekee.

Dan Coats pia hakukubaliana na suala la Korea Kaskazini.

Donald Trump, ambaye alionekana kuwa ma mashaka na mkuu wake wa Ujasusi, alimtenga katika faili kadhaa.

Alimshukuru Dan Coats kwenye ukurasa wake wa Twitter kwa "kazi kubwa alizofanya kwa nchi yetu". Kisha akatangaza haraka kwenye Twitter nia yake ya kumteua John Ratcliffe, kuchukuwa nafasi yake.

Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu Mkuu wa polisi ya mipaka nchini Marekani, John Sanders, alitangaza kuachia ngazi baada ya kugundulika kwamba watoto wahamiaji wanazuiliwa katika mazingira mabaya, hali ambayo ilifichuliwa kwa vyombo vya habari.