MAREKANI-USALAMA

Wanne wauawa katika shambulio wakati wa tamasha California

Watu wanne ikiwa ni pamoja na mshambuliaji wameuawa katika shambulio la watu wenye silaha wakati wa tamasha katika eneo la Gilroy, California, kusini mwa San Francisco, nchini Marekani.

Maafisa wa Idara ya huduma ya dharura kwenye eneo la tukio, Gilroy, Julai 28, 2019.
Maafisa wa Idara ya huduma ya dharura kwenye eneo la tukio, Gilroy, Julai 28, 2019. REUTERS/Chris Smead
Matangazo ya kibiashara

"`Rambirambi zetu na za jamii nzima tunazitoa kwa wahasiriwa wa shambulio la leo kwenye Tamasha la Garlic," polisi wa eneo hilo imeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kwa mujibu wa diwani wa jiji hilo, Dion Bracco, akinukuliwa na vyombo kadhaa vya habari nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na gazeti la New York Times, watu watatu wameuawa katika shambulio hilo. Mshambuliaji wa shambulio hilo pia ameuawa kwa risasi, kwa mujibu wa polisi.

Picha kutoka NBC News zinaonyesha washiriki wa tamasha hilo walivyokuwa wakikimbia wakati milio ya risasi iliyokuwa ikisikika kwenye jumba ambako kulikuwa kukifanyika tamasha la Gilroy Garlic, moja ya tamasha kubwa la chakula nchini, kilomita 48 kusini mashariki mwa San Jose.

Idhaa hiyo pia iliripoti ushuhuda wa mwanamke, Julissa Contreras, akisema aliona mzungu , mwenye umri wa miaka 30 akifyatua risasi dhidi ya umati wa watu.

Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na shambulio hilo, lakini polisi inasema uchunguzi unaendelea.