BRAZILI-USALAMA-HAKI

Brazili: Wafungwa 57 waangamia katika machafuko kati ya makundi hasimu

Maafisa wa jeshi la polisi mbele ya gereza la Manaus, Brazil (Picha ya kumbukumbu).
Maafisa wa jeshi la polisi mbele ya gereza la Manaus, Brazil (Picha ya kumbukumbu). REUTERS/Ueslei Marcelino

Hali ya wasiwasi inaendelea kutanda katika jela la Altamira, Kaskazini mwa Brazili, baada ya wafungwa 57 kuuawa Jumatatu wiki hii katika makabiliano kati ya makundi hasimu.

Matangazo ya kibiashara

Hali hii inaendelea kujitokeza katika eneo hili la kimkakati ambako makundi hasimu ya wahalifu yanaendelea kupigana kuhusu biashara ya madawa ya kulevya aina ya kokaini.

Mamlaka ya magereza imebaini kwamba wafungwa 16 wamepatikana wamekatwa vichwa.

Uhasama huo, ambao ulianza karibu 7:00 asubuhi saa za Brazili (sawa na saa 10:00 sa za kimataifa) katika jela la Altamira katika Jimbo la Para, katikati mwa msitu wa Amazon, ulimalizika mapema mchana.

"Askari magereza wawili walitekwa, lakini waliachiliwa haraka kwa sababu lengo ilikuwa ulipizaji kisasi kati ya makundi hasimu na sio ghasia za kupinga mazingira ya kizuizini" Gavana wa Para, Jarbas Vasconcelos, amesema, akinukuliwa katika taarifa kutoka kwa viongozi wa eneo hilo.

Wafungwa kutoka kundi la wahalifu waliingia katika sehemu walikokuwa wanafungwa wafungwa wa kundi jingine hasimu kabla ya kuwachoma moto.

"Inawezekana kwamba wafungwa wengi wamefariki dunia kwa kukosa hewa," amesema msemaji wa mamlaka ya magereza, na kuongeza kuwa wataalam walikuwa eneo la tukio na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka.

Video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha vichwa sita vya wafungwa vimewekwa karibu na ukuta.

Wizara ya sheria nchini Brazil imesema kuwa mchakato wa kuwahamisha wafungwa waliohusika na ghasia hizo kwenda jela mbalimbali umeanza.

Waziri Sergio Moro amesema anasikitishwa na vifo hivyo na kutangaza kwamba ana imani kuwa hali hiyo haitojirudi tena katika magereza, kwani usalama wa kutosha utaimarishwa.