MAREKANI-TRUMP-ZELENSKIY-SIASA

Wabunge nchini Marekani waanza mchakato wa kuchunguza iwapo Trump aondolewe madarakani

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akikutana na rais wa Marekani Septemba 25 2019 jijini New York
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akikutana na rais wa Marekani Septemba 25 2019 jijini New York ©REUTERS/Jonathan Ernst

Wabunge nchini Marekani, wameanza mchakato wa kuchunguza uwezekano wa kumdoa madarakani rais Donald Trump baada ya mazungumzo yake ya simu na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, mwezi Julai, akimtaka kumchunguza aiyekuwa Makamu wa rais Joe Biden kwa madai ya ufisadi, kwa sababu za kisiasa.

Matangazo ya kibiashara

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa idara ya usalama nchini humo Joseph Maguire amekuwa mbele ya Kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya Inteljensia, kuwaelezea kile anachofahamu kuhusu mazungumzo ya rais Trump na mwenzake wa Ukraine.

Maguire katika maelezo yake amesema hafahamu aliyevujisha mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, huku akitetea uamuzi wake kutoweka suala hili wazi na kusisitiza kuwa halikutokea katika ofisi yake.

Alipoulizwa iwapo aliwahi kuonana na kuzungumza na rais Trump kuhusu suala hili, Mkuu huyo wa usalama alijibu kuwa yeye, huonana mara kwa mara na rais Trump lakini sio kuhusu hili.

Rais Donald Trump ameelezea sakata hili, kama utapeli mkubwa katika historia ya siasa za Marekani.

Uchaguzi nchini Marekani ni mwaka ujao na wachambuzi wa siasa wanaona huenda akakabiliwa na upinzani iwapo Makamu wa zamani wa rais Joe Biden atapata tiketi ya chama chake kuwania nafasi hiyo.