MAREKANI-SIASA

Mkosoaji mkubwa wa Trump na mbunge wa chama cha Democratic afariki dunia Marekani

Elijah Cummings Agosti 7, 2019 Washington.
Elijah Cummings Agosti 7, 2019 Washington. © AFP

Elijah Cummings, mbunge wa chama cha Democratic, na mkosoaji mkubwa wa Rais wa Marekani Donald Trump, amefariki dunia leo Alhamisi nchni Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Elijah Cummings ambaye alikuwa na nafasi muhimu katika uchunguzi kuhusu kutimuliwa kwa Rais Donald Trump, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 68, kulingana na taarifa ya ofisi yake.

Mbunge huyo wa Maryland aliyechaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi amefariki katika Hospitali ya Johns Hopkins katika mji wa Baltimore.

"Elijah Cummings aliugua kwa muda mrefu," kulingana na taarifa.

Elijah Cummings, mbunge mweusi kwenye Baraza la Wawakilishi, ambapo alihudumu tangu mwaka 1996, na mwenyekiti wa tume ya usimamizi wa serikali, alilikuwa na jukumu muhimu katika uchunguzi wa rais wa Marekani, ambaye wabunge kutoka chama cha Democratic wanataka kumng'atua madarakani. Mara nyingi alikuwa akimpinga rais wa Marekani katika miezi ya hivi karibuni.

"Nimepatwa na huzuni mkubwa na mfadhaiko baada ya kupata taarifa ya kifo chake, " amesema Chuck Schumer, kiongozi wa maseneta kutoka chama cha Democratic, walio wachache katika baraza hilo la Seneti, huku akisema wamepata "hasara kubwa."

"Leo tumepoteza mtu mkubwa," amesema seneta Kamala Harris kutoka California. Elijah Cummings alikuwa "kiongozi jasiri, mlinzi wa demokrasia yetu," ametangaza Kamala Harris.