MAREKANI-TRUMP-SIASA-HAKI

Bunge kupiga kura kuongeza shinikizo katika uchunguzi dhidi ya Trump

Donald Trump amepiga marufuku wajumbe wa utawala wake kujibu hoja za Baraza la Wawakilishi.
Donald Trump amepiga marufuku wajumbe wa utawala wake kujibu hoja za Baraza la Wawakilishi. REUTERS/Leah Millis

Utaratibu wa kumtimuwa madarakani Donald Trump ulioanzishwa hivi karibuni, unaingia leo Alhamisi katika hatua mpya. Baraza la Wawakilishi linatarajia Alhamisi wiki hii kupiga kura kuongeza uzito katika uchunguzi huu unaomkabili rais wa Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Kura hii itawawezesha wabunge kuwahoji hadharani mashahidi wa kesi hiyo ya mazungumzo ya simu baina ya rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Ukraine.

Mazungumzo hayo ya simu yamewafanya wabunge kutoka chama cha upinzani cha Democrats kuanzisha uchunguzi rasmi wenye lengo la kumng'oa madarakani bw Trump.

Wabunge wa Democrats wanamshutumu Trump kwa kutaka usaidizi kutoka kwa taifa la kigeni ili kumuangamiza hasimu wake wa kisiasa.

Taarifa ya White House inathibitisha kuwa, mnamo Julai 25, Trump alimuomba rais Volodymyr Zelenski kumchunguza makamo wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden ambaye anasaka tiketi ya urais kupitia chama cha Democrats, ambaye mtoto wake alikuwa akifanya kazi na shirika la gesi la Ukraine.

Bw Trump anakanusha kuwa alizuia msaada wa kijeshi kwa Ukraine kama njia ya kuishinikiza nchi hiyo kumsaidia kumchafua adui wake wa kisiasa, bw Biden.

Taarifa juu ya mazungumzo hayo ya simu yametolewa na mtoa taarifa wa siri.

Huku kukiwa na uungaji mkono mkubwa kutoka kwa wafuasia wa Democrats juu ya uchunguzi huo unaoweza kumuondoa mamlakani , ikiwa utaendelea huenda usipitishwe na baraza la seneti - linalodhibitiwa na wabunge wa chama cha Trump cha Republican.

Hivi karibuni Bwana Trump alikiri kuwa alimzungumzia Joe Biden na Bwana Zelensky lakini akasema alikuwa tu akijaribu kuitaka Ulaya iingilie kati kutoa msaada kwa kuitishia kusitisha msaada wa kijeshi.