Pata taarifa kuu
BOLIVIA-SIASA-USALAMA

Rais wa Bolivia Evo Morales aachia ngazi

Rais Evo Morales akitangaza kujiuzulu kwake Novemba 10, 2019.
Rais Evo Morales akitangaza kujiuzulu kwake Novemba 10, 2019. HO / Bolivia TV / AFP
Ujumbe kutoka: RFI
Dakika 2

Rais wa Bolivia Evo Morales ameamua kuachia ngazi kwenye uongozi wa nchi, baada ya wiki tatu za maandamano makubwa dhidi ya kuchaguliwa kwake tena kwa muhula wa nne. Hatua hiyo imekuja wakati jeshi na polisi walikuwa wamemtaka aondoke madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya wiki tatu za maandamano makubwa na kupoteza imani kwa jeshi, Hatimaye Evo Morales ameaamua kujiuzulu kwenye wadhifa wake wa urais wa Bolivia.

"Ninaachia nafasi yangu kama rais," kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60, ambaye amekuwa madarakani tangu 2006, amesema kwenye runinga ya taifa Jumapili Novemba 10.

"Jaribio la mapinduzi limefanyika," ameongeza Makamu wa rais Alvaro Garcia Linera, ambaye pia amejiuzulu.

"Tumezindua somo kwa ulimwengu, kesho Bolivia itakuwa nchi mpya," amebaini rais wa zamani Carlos Mesa, kiongozi wa upinzaji na mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 20, wakati maelfu ya wananchi wa Bolivia walikuwa wakisherehekea mitaani hatua hiyo ya kujiuzulu kwa rais Evo Morales na makamu wake Alvaro Garcia Linera.

Raia walikuwa wakipinga serikali waliingia mitaani na kusherehekea ushindi wao.

Saa moja kabla ya hatua hiyo ya kujiuzulu, Mkuu wa majeshi ya Bolivia alikuwa amemtaka rais Evo Morales kung'atuka madarakani.

"Baada ya kutathmini hali ya mzozo wa ndani unaoendelea, tunamwomba rais ang'atuke madarakani ili amani na usalama viweze kutawala, kwa faida ya Bolivia yetu," Jenerali Williams Kaliman aliwaambia waandishi wa habari.

"Tunajiunga na wito wa wananchi wa Bolivia wa kumpendekeza rais Evo Morales kujiuzulu ili kuunganisha wananchi wa Bolivia," kamanda mkuu wa polisi, Jenerali Vladimir Yuri Calderon alisema.

Rais wa Cuba, ambaye ni mshirika wa karibu wa Evo Morales alitangaza hatua hiyo ya kujiuzulu kwa Evo Morales akilaani "jaribio la mapinduzi nchini Bolivia". Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Miguel Diaz-Canel amesema "anashikamana na ndugu rais Evo Morales" na ameomba jumuiya ya kimataifa kushinikiza mamlaka nchini Bolivia"kuhusu uhuru na usalama wa Evo Morales".

Hata Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amelaani "jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala wa Evo Morales na kuitaka jamii ya kimataifa kuingilia kati usalama na uhuru wa Evo Morales.

Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.