MAREKANI-TRUMP-KURA-SIASA

Wabunge nchini Marekani kupiga kura kumwondoa rais Trump madarakani

Wabunge nchini Marekani wanajiandaa kupiga kura ya kukosa imani na rais Donald Trump baadaye siku ya Jumatano huku wabunge wa chama cha Democratic wakitarajiwa kupitisha mswada huo.

Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi, akiwa na rais Donald Trump mapema mwaka 2019 wakati akihotubia wabunge
Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi, akiwa na rais Donald Trump mapema mwaka 2019 wakati akihotubia wabunge REUTERS/Leah Millis
Matangazo ya kibiashara

Hii ni hatua ya kihistoria, na rais Trump anakuwa rais wa tatu katika historia ya Marekani kupIia mchakato huu ambao umewagwa wabunge wa chama cha Democratic na Republican.

Rais Trump, anashtumiwa kwa kutumia vibaya madaraka yake na hatua hii imekuja, baada kuwa na mawasiliano na rais wa Ukraine, na kutaka kuchunguzwa kwa mpinzani wake wa kisiasa makamu wa rais wa zamani Joe Biden.

Kuelekea hatua hii, rais Trump amemwandikia barua spika wa bunge Nancy Pelosi na kumwambia historia itamhukumu vikali na kusisitiza kuwa hana kosa.

“Ni aibu kumwondoa madarakani rais wa Marekani kwa madai kama haya, nimefanya kazi kubwa ndnai ya miaka hii mitatu, kinachoendelea kisipokosolewa, huenda kikatokea kwa rais mwingine ambaye atakuwa na maoni tofauti,” alisema rais Trump.

Hata hivyo, Maseneta wa chama cha rais Trump, wanatarajiwa kuzuia kuondolewa madarakani kwa rais Trump kwa sababu ni wengi dhidi ya wale wa Democratic.

Wachambuzi wa siasa wanasema, kinachoendelea Marekani ni harakati za kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, uchaguzi ambao rais Trump anatarajiwa kuwania tena kwa muhula wa pili na wa mwisho.