MAREKANI-UKRAINE-TRUMP-SIMU

Marekani ilisitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine baada ya simu ya Trump

Rasi wa Marekani Donald Trump
Rasi wa Marekani Donald Trump BRENDAN SMIALOWSKI / AFP

Ikulu ya Marekani iliagiza kusitishwa kwa msaada wa kijeshi kwa nchi ya Ukraine, dakika 91 tu baada ya rais Donald Trump kuzungumza na mwenzake wa Volodymyr Zelensky kwa njia ya simu mwezi Julai.

Matangazo ya kibiashara

Hii imethibitishwa kupitia barua pepe ya serikali iliyotolewa  wazi kwa umma na kuzua mjadala mpya kuhusu mazungumzo hayo tata ya rais Trump.

Katika mazungumzo hayo ya simu, rais Trump alimtaka kiongozi huyo wa Ukraine kumchunguza mpinzani wake wa kisiasa, aliyekuwa Makamu wa rais Joe Biden.

Wabunge wa chama cha Democratic wanasema, barua hiyo inaonesha kuwa rais Trump alitumia madaraka yake kwa maslahi binafsi na inathibitisha mashtaka dhidi yake.

Mazungumzo kati ya rais Trump na Zelensky yamesababisha wabunge wa chama cha Democratic katika bunge la wawakilishi kupiga kura ya kukosa imani na rais Trump.

Baada ya hatua hiyo, hatima yake sasa ipo mikononi mwa bunge la Senate na kwa sababu chama cha Republican kina Maseneta wengi, ni wazi kuwa watamlinda Trump wakati wa zoezi hilo mwezi Januari  ikiwa na maana kuwa ataendelea kuwa madarakani.

Trump amekuwa akikanusha mashtaka dhidi yake na kusema yanatumiwa kisiasa, kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.