IRAN-MAREKANI-IRAQ-USALAMA

Iran yaapa kulipiza kisasi shambulizi la Marekani Iraq

Mmoja wa waandamanaji akishikilia mikononi picha ya Ayatollah Ali Khamenei akiwa pamoja na jenerali Qassem Soleimani (kushoto) wakati wa maandamano dhidi ya shambulizi la Marekani, Baghdad, Januari 3, 2020.
Mmoja wa waandamanaji akishikilia mikononi picha ya Ayatollah Ali Khamenei akiwa pamoja na jenerali Qassem Soleimani (kushoto) wakati wa maandamano dhidi ya shambulizi la Marekani, Baghdad, Januari 3, 2020. WANA (West Asia News Agency)/Nazanin Tabatabaee

Iran imeapa kulipiza kisasi shambulizi la anga la Marekani lililomuua afisa mwandamizi wa jeshi , Jenerali Qassem Soleimani, ambaye alikuwa mkuu wa Jeshi maalum la Iran.

Matangazo ya kibiashara

Jenerali Soleimani aliuawa pamoja na Abu Mahdi al-Muhandis, naibu kamanda wa wanamgambo wa Iraq wa Popular Mobilization Forces - PMF wanaoungwa mkono na Iran, na watu wengine watano baada ya msafara wao kulengwa katika shambulizi la angani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad.

Kiongozi wa juu kabisa wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameonya kuwa watachukua hatua kali za kulipiza kisasi. Ametangaza siku tatu za maombolezi kufuatia kifo hicho.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Javad Zarif, ametaja hatua hiyo kuwa "hatari na uchokozi wa kishenzi".

Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema Rais Donald Trump aliamuru kuuawa kwa Soleimani baada ya kundi la waandamanaji wanaoiunga mkono Iran kuuzingira ubalozi wa Marekani.

Kuuawa kwa Jenerali Qassem Soleimani, mkuu wa Jeshi maalum la Iran, kunaashiria kuongezeka kwa mgogoro kati ya Marekani na Iran, ambao umekuwa ukitokota tangu Rais Donald Trump alipojiondoa katika mkataba wa nyuklia wa Iran na kutangaza vikwazo vipya vinavyohujumu uchumi wa nchi hiyo.

Baada ya sala ya Ijumaa, umati wa watu wamefurika kwenye mitaa ya katikati mwa mji mkuu wa Irani, Tehran, wakishikilia mikononi picha za Qassem Soleimani, huku wakitoa maneneo makali dhidi ya Marekani.

Jenerali Soleimani alikuwa mtu mashuhuri kwa utawala wa Iran. Kikosi chake cha Qudsi kilikuwa kinaripoti moja kwa moja kwa kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na alisifiwa kama shujaa wa kitaifa.