MAREKANI-UCHAGUZI-SIASA

Kura za mchujo katika chama cha Democratic: Joe Biden amuangusha Sanders katika majimbo kadhaa

Nchini Marekani, matokeo ya kwanza ya "Jumanne maalum" kuhusu kura za mchujo kwa wagombea urais katika chama cha Democratic yanaendelea kutolewa kwa upande mmoja baada ya mwingine.

Bernie Sanders na Joe Bien wakati wa mjadala kati ya wagombea wa urais katika kura za mchujo katika chama cha Democratic Februari 25, 2020 huko Charleston, South Carolina.
Bernie Sanders na Joe Bien wakati wa mjadala kati ya wagombea wa urais katika kura za mchujo katika chama cha Democratic Februari 25, 2020 huko Charleston, South Carolina. Win McNamee/Getty Images/AFP
Matangazo ya kibiashara

Kura zimepigwa katika majimbo kumi na nne ili kumchagua mgombea atakayepepetana na Donald Trump katika uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu. Wagombea katika uchaguzi huo ni kati ya Bernie Sanders, seneta kutoka Vermont, na Joe Biden, makamu wa rais wa zamani wa Barack Obama.

Joe Biden amenyakua ushindi katika majimbo ya Alabama, Arkansas, North Caroline, Massachusetts, Minnesota, Oklahoma, Tennessee na Virginia.

Naye Bernie Sanders anaongoza katika majimbo ya Colorado, Utah na Vermont. Hivi sasa ndiye anaongoza katika majimbo ya California na Texas.

Kwa upande mwengine Elizabeth Warren ameanguka katika ngome yake ya Massachussets, huku Joe Biden akiibuka mshindi katika jimbo hilo, kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Marekani.

Makamu wa rais wa zamani, ambaye hadi hivi sasa anakabiliwa na upinzani mkubwa tangu kuanza kwa kura hizi za mchujo, amefanya vizuri katika majimbo nane wakati wa zoezi hilo la "Jumanne maalum", ambapo kwa jumla majimbo 14 yamepiga kura.

Jumla ya wajumbe 1,357 wanashindaniwa katika uchaguzi huu wa Jumanne Maalum, na Biden anahitaji matokeo mazuri ili kumzuia Sanders kuchukua uongozi mkubwa kabla ya mkutano mkuu wa chama utakaomteuwa mgombea wa chama mwezi Julai.

Wengi katika chama cha Democratic wana hamu ya kuizuia kasi ya Sanders katika kura hizi za wajumbe, wakisema seneta huyo atashindwa vibaya kabisa katika uchaguzi mkuu ambao Trump amedokeza kuwa atamuita kuwa msoshalisti anayetaka kuuwekea kikomo mtindo wa maisha ya Wamarekani.

Meya wa zamani wa New York Michael Bloomberg na Seneta wa Massachusetts Elizabeth Warren pia wanashiriki katika kinyang'anyiro hiki.