PERU-FUJIMORI-HAKI

Peru: Kiongozi wa upinzani Keiko Fujimori aachiliwa huru

Keiko Fujimori akiondoka jela la Wanawake huko Lima Mei 4, 2020.
Keiko Fujimori akiondoka jela la Wanawake huko Lima Mei 4, 2020. REUTERS/Sebastian Castaneda

Mahakama ya Rufaa nchini Peru imechukuwa uamuzi wa kumuachilia huru kiongozi wa upinzani Keiko Fujimori, baada ya kuzuiliwa miezi mitatu akishtumiwa makosa ya ufisadi katika kesi ya Odebrecht.

Matangazo ya kibiashara

Akivalia barakoa, binti mkubwa wa rais wa zamani wa Peru Alberto Fujimori (1990-2000) aliondoka Jumatatu wiki hii katika gereza la wanawake la Chorrillos, Kusini mwa Lima, na alitumia usafiri wa taxi kwenda nyumbani.

Hawezi kuondoka katika mji wa Lima bila idhini ya mahakama na anatakiwa kuripoti mahakani mara moja kwa mwezi.

Mei 1, 2020 Mahakama ya Rufaa iliaagiza Keiko Fujimori aachiliwe huru kwa dhamana ya fedha za Peru 70,000 (karibu euro 19,000) na kwa sharti la kutoishi na mumewe, Marko Vito Villanella, raia wa Marekani, anayehusishwa katika uchunguzi huo wa ufisadi.

Keiko Fujimori, 44, hivi karibuni aliomba kuachiliwa kwa dhamana kwa sababu ya hatari ya kuambukizwa virusi vya Corona katika jela. Lakini mahakama imejibu ombi la awali lililotolewa na wanasheria wake.

Kabla ya kuondoka jela, Keiko Fujimori alionyesha nia yake ya kufanya vipimo vya Corona kabla ya kuwasiliana na familia yake.