VENEZUELA-MAREKANI-USALAMA

Venezuela: Wamarekani wawili wakamatwa kwa 'uvamizi wa kijeshi'

Wanajeshi wa Venezuela wamewakamata watu kadhaa - ikiwa ni pamoja na Wamarekani wawili - ambao watuhumiwa kujaribu kuvamia kijeshi nchi hiyo, Mei 4, 2020.
Wanajeshi wa Venezuela wamewakamata watu kadhaa - ikiwa ni pamoja na Wamarekani wawili - ambao watuhumiwa kujaribu kuvamia kijeshi nchi hiyo, Mei 4, 2020. VENEZUELAN GOVERNMENT TV/Handout via REUTERS TV

Rais wa Venezuela ametangaza kwamba mamlaka ya nchi yake imewakamata "magaidi" 13, ikiwa ni pamoja na raia wawili wa Marekani ambao amewataja kuwa ni mamluki, kwa kuhusika kwao katika jaribio lililotibuliwa, ambalo amesema lengo lake ilikuwa kumuondoa madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Katika hotuba iliyorushwa kwenye runinga ya serikali VTV, Nicolas Maduro amemshtmu moja kwa moja Juan Guaido kuhusika na kitendo hicho.

Kwa mujibu wa rais wa Venezuela, kiongozi huyo wa upinzaji aliajiri "mamluki" kutoka kwa vikosi maalum vya Marekani ili kujaribu "kuvamia" nchi hiyo kwa lengo la kuipindua serikali yake.

Nicolas Maduro ameonyesha pasi za kusafiria za Wamarekani hao wawili, Luke Denman, 34, na Airan Berry, 41. Rais Maduro amebaini kwamba wawili hao ni wafanyakazi wa Silvercorp, kampuni ya ulinzi, yenye makao yake makuu huko Florida, ambapo mmiliki wa kambuni hiyo amekiri jaribio la uvamizi, ameongeza Nicolas Maduro.

Jordan Goudreau ameliambia shirika la habari la Reuters mapema Jumatatu kwamba raia hao wawili wa Marekani wanaofanya kazi katika kampuni yake wanashikiliwa na mamlaka ya Venezuela. "Hao ndio ni wafanyakazi wangu," askari huyo wa zamani wa Jeshi la Marekani amesema katika mahojiano kwa simu.

Kulingana na tovuti ya kampuni ya Silvercorp, Goudreau ni "askari mstaafu aliyetunukiwa tuzo nyingi kutoka vikosi maalum vya Marekani" ambaye alipigana nchini Iraq na Afghanistan.

Siku ya Jumapili, serikali ya Venezuela ilitangaza kwamba mamluki hao walijaribu kuingia nchini humo kupitia boti zinazotembea kwa kasih kutoka Colombia, akilaani kitendo kinachoungwa mkono na Marekani.

Marekani haijazungumza chochote kuhusiana na madai hayo ya Caracas.

Timu ya mawasiliano ya Guaido imefutilia mbali ripoti za waandishi wa habari zinazosema kwamba kiongozi wa upinzaji alikuwa amemtaka Silvercorp kumtimua madarakani Nicolas Maduro.