MAREKANI-CHINA-POMPEO-CORONA-AFYA

Coronavirus: Pompeo aituhumu Beijing kuhusika kwa mamia ya maelfu ya vifo

Waziri wa Mashauriano ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo ameinyooshea kidolea cha lawama China kwa jinsi ilivyoshughulikia mlipuko wa virusi vya corona
Waziri wa Mashauriano ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo ameinyooshea kidolea cha lawama China kwa jinsi ilivyoshughulikia mlipuko wa virusi vya corona REUTERS/Yuri Gripas

Waziri wa Mashauriano ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo, kwa mara nyingine ameikosoa vikali China, akiishtumu kuhusika kwa mamia ya maelfu ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa hatari wa Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

"Walijua," Mike Pompeo amesema wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kwenye makao makuu ya Wizara ya Mashauriano ya Kigeni. "China ingeweza kuzuia vifo vya mamia ya maelfu ya watu ulimwenguni kote. China ingeliokoa ulimwengu kutokana na kuingia kwenye mtikisiko mkubwa wa uchumi."

Mike Pompeo ameongeza kuwa China "bado inakataa kutoa taarifa tunazozihitaji kulinda raia."

Mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 umeuwa watu zaidi ya 255,000 ulimwenguni kote, ikiwa ni pamoja na zaidi ya 70,000 nchini Marekani, ambayo ni nchi iliyoathiriwa zaidi na mgogoro huu wa kiafya.

Mapema wiki hii rais wa Marekani Donald Trump aliulezea ugonjwa wa Covid-19 kuwa ni "shambulio" baya zaidi hali jawahi kutoka nchini Marekani.

Jumuiya ya wanasayansi wanakubaliana kwamba virusi vya Corona, ambavyo vilianzia katika mji wa China wa Wuhan mwishoni mwa mwaka jana, vilitokea katika soko wanakouza wanyama wa porini na kisha kuenea kwa binadamu.

Hivi karibuni Mike Pompeo alisema kwamba ana ushahidi mzuri unaoonyesha kuwa virusi hivyo vilitoka kwa maabara moja nchini China.