Trump kupunguza idadi ya askari wa Marekani Ujerumani
Imechapishwa:
Rais wa Marekani Donald Trump amtangaza kwamba anataka kupunguza nusu ya wanajeshi Marekani walioko nchini Ujerumani, akibaini kwamba Berlin ina "malimbikizo" katika michango yake ili kufadhili shughuli za Jumuiya ya Kujihami ya NATO.
Rais Trump pia amebaini kwamba Ujerumani haina uhusiano mzuri katika masuala ya biashara na Marekani.
Rais wa Marekani amewahakikishia waandishi wa habari kwamba wanajeshi 52,000 wa Marekani sasa wako nchini Ujerumani. "Ni gharama kubwa kwa Marekani," Donald Trump ameongeza. "Kwa hivyo tutapunguza idadi ya askari wetu, hadi 25,000, " rais Trump amebaini.
Kuna kati ya wanajeshi 34,000 na 35,000 pekee wa kudumu walioko Ujerumani, kulingana na takwimu rasmi kutoka Pentagon. lakini, idadi hii inaweza kuongezeka hadi 52,000 kutokana na kuwa kuna askari wengi ambao walikuja kufuata mafunzo ya kijeshi nchini humo.
Wanajeshi wa Marekani wamekuwepo Ujerumani tangu mwisho wa Vita Vikuu vya Pili duniani, ambapo walikuwa sehemu kubwa ya wanajeshi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO dhidi ya muungano wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi.
Kuibuka tena kwa malengo ya kijeshi ya Urusi chini ya Rais Vladimir Putin, kuliipa Marekani umuhimu wa wanajeshi wake kuwepo Ujerumani kwa miongo miwili iliyopita, huku nchi za kati na mashariki mwa Ulaya zikishinikiza kuimarishwa kwa ushirikiano thabiti na Marekani.