Fauci aonya Marekani kukumbwa na mlipuko mpya wa Corona
Imechapishwa:
Daktari Anthony Fauci, afisa wa juu na mtalaam wa magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani amewaambia wabunge nchini humo kuwa, kuna wasiwasi wa kuendelea kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona katika baadhi ya majimbo nchini humo.
Aidha, ameonya kuwa hali ikiendelea hivi, idadi ya maambukizi itaongezeka sana na hata kushuhudiwa kwa mlipuko mpya wa virusi hivyo.
Fauci pia amewasihi raia kujiepusha na mikusanyiko mikubwa na kuvaa barakoa wakati wakiwa karibu na watu wengine kujaribu kuzuia kuongezeka kwa maambukizi hayo, wakati Trump akiendelea kupuuza ushauri wa namna hiyo, na kufanya mikutano ya hadhara.
Marekani kwa sasa ina maambukizi ya watu zaidi ya Milioni mbili huku wengine zaidi ya Laki Moja na Elfu Ishirini wakipoteza maisha.
Marekani inakabiliwa na kipindi kigumu, wakati Umoja wa Ulaya Jumanne uliitishia kuwazuia raia wa nchi hiyo kuingia kwenye mataifa yake, kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona katika majimbo tofauti ya Marekani, hususan Florida, Arizona na Texas.