BRAZILI-CORONA-AFYA

Brazil: Rais Bolsonaro atangaza kuwa ameambukizwa Corona

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro akivaa barakoa katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano Machi 18 huko Brasilia.
Rais wa Brazil Jair Bolsonaro akivaa barakoa katika mkutano na waandishi wa habari Jumatano Machi 18 huko Brasilia. Sergio LIMA / AFP

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amethibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona siku ya Jumanne,baada ya vipimo vinne ,vilivyochukuliwa baada ya rais huyo kuonesha dalili za Corona, ikiwemo joto jingi mwilini.

Matangazo ya kibiashara

Rais Bolsonaro amenukukuliwa akipinga vikali kuwepo hatari ya ugonjwa huo na kugoma kutangaza kusitisha shughuli za kawaida akisema hatua hiyo ingeathiri mno uchumi.

"Majibu ya vipimo yamewasili, nimekutwa nimeambukizwa virusi vya Corona," rais wa Brazili amesema katika mahojiano na vituo kadhaa vya televisheni, baada ya kupata homa kali siku moja iliyopita.

"Nilikuwa na homa ya digrii 38, lakini mapafu yangu yalikuwa safi. Madaktari walinipa hydroxychloroquine na azithromycin na baada ya hapo nilipata nafuu. Niko sawa, ”ameongeza Rais Jair Bolsonaro. Amesema sasa atafanya kazi iwezekanavyo "kupitia video".

Rais Bolsonaro amekuwa akipuuzia mbali hatari ya Corona, na nchi yake sasa ni miongoni mwa mataifa yaliyoathirika mno, ikiwa imeripoti visa zaidi ya milioni moja na sita na vifo elfu 65.

Rais Bolsonaro ambaye mara kwa mara amekuwa akikataa kuvaa barakoa amesema pia amechunguzwa mapafu kwa kutumia kipimo cha picha cha X-ray katika hospitali ya kijeshi kama tahadhari.

Brazili inaendelea kushikilia nafasi ya pili kwa vifo zaidi duniani vinavyohusiana na janga la Covid-19 baada ya Marekani ambayo inaongoza kwa visa zaidi ya Milioni 2 vya maambukizi.

Brazili, ambayo ni nchi kubwa katika ukanda wa Amerika ya Kusini (yenye wakaazi milioni 212) pia ni ya pili kwa idadi kubwa ya maambukizi yaliyothibitishwa nyuma ya Marekani, ikiwa na visa Milioni 1,67 vya maambukizi, baada ya visa 45 305 kuthibitishwa. Watu 66,868 wamefariki dunia baada ya vifo vipya 1,254 kuthibitishwa katika muda wa saa 24.