MAREKANI-WHO-CORONA-AFYA

Marekani yaanza mchakato wa kujitoa WHO

Rais Donald Trump aliishutumu WHO kwa kutoshirikishana taarifa zinazoonyesha maambukizi ya virusi vya Corona kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine yaliyokuwa yakijiri nchini China.
Rais Donald Trump aliishutumu WHO kwa kutoshirikishana taarifa zinazoonyesha maambukizi ya virusi vya Corona kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine yaliyokuwa yakijiri nchini China. SAUL LOEB / AFP

Rais wa Marekani Donald Trump ameanza mchakato wa kuiondoa rasmi nchi yake kwenye uanachama wa shirika la Afya duniani WHO, miezi kadhaa baada ya rais Trump kutishia kufanya hivyo.

Matangazo ya kibiashara

Trump mwezi wa Mei aliweka bayana nia hiyo akiishtumu WHO kwa kutumika na China katika mapambano ya Corona, na sasa ameandikia Umoja wa Mataifa na bunge la Congress kuhusu mchakato huo.

Kujiondoa huko kwa Marekani kumepangwa kufanyika Julai 6 mwakani, kwa mujibu wa vyanzo kadhaa.

Rais Donald Trump alilishutumu shirika la Afya Duniani kwa kuruhusu ugonjwa wa Covid -19 kushindwa kudhibitika na kupuuzia hatari ya ugonjwa huo, ambao umesababisha vifo vya maelfu ya watu duniani.

Rais Trump aliilaumu China kwa kujaribu kuziba mlipuko huo na kuishtumu WHO kwa kushindwa kuiwajibisha China.

Pia alilishutumu shirika hilo kwa “kuipendelea China”, sehemu ya shutuma hizo zikiwa ni kutokana na upingaji wake mkali wa hatua ya Marekani kuwazuia wasafiri kutoka China kuingia nchini humo.

Mwezi Mei Rais Trump alitangaza kwamba Marekani itasitisha kulichangia shirika hilo na kutumia fedha hizo kwa ajili ya shughuli zingine.

Marekani ni mchangiaji mkubwa wa WHO. Taarifa rasmi ya kujiondoa huenda ikaathiri juhudi za dunia za kupambana na maambukizi ya virusi hivyo.