MAREKANI-CORONA-AFYA-SIASA

Marekani yaweka rekodi mpya ya maambukizi mengi ya Corona

Mnamo Jumatano, mtaalamu na pia mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza nchini humo Daktari Antony Fauci, alisema haelewi juhudi za baadhi ya maafisa wa Ikulu ya White House kumdharau lakini anaamini hilo ni kosa kubwa.
Mnamo Jumatano, mtaalamu na pia mkuu wa idara ya magonjwa ya kuambukiza nchini humo Daktari Antony Fauci, alisema haelewi juhudi za baadhi ya maafisa wa Ikulu ya White House kumdharau lakini anaamini hilo ni kosa kubwa. POOL / GETTY IMAGES NORTH AMERICA / Getty Images via AFP

Marekani imeweka rekodi nyingine mpya ya maambukizi mengi ya corona ya kila siku, hasa Kusini mwa nchi hiyo, wakati India imechukuwa hatua kuwaweka karantini watu Milioni 125.

Matangazo ya kibiashara

Marekani, nchi ambayo imeathirika zaidi duniani, imeweka rekodi mpya ya maambukizi mengi ya Corona kwa muda wa saa 24 Jumatano wiki hii, ambapo visa vipya zaidi ya 67,000 vya maambukizi vimethibitishwa, Kulingana na takwimu za chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Jimbo la Texas pekee limerekodi visa vipya 10,790, maafisa wa afya wameripoti.

Marekani, moja ya nchi zenye nguvu duniani inaendelea kukabiliwa maambukizi zaidi ya virusi vya Corona tangu mwishoni mwa mwezi Juni, hasa katika majimbo ya kusini na magharibi mwa nchi. Kwa kipindi cha siku kumi, idadi ya maambukizi kwa kila baada ya saa 24 ni kati ya 55,000 na 65,000.

Hayo yanajiri wakati Rais Donald Trump na Antony Fauci, mtaalamu mkuu wa serikali kuhusu masuala ya Corona hawaafikiani kuhusu jinsi ya kukabiliana na janga hilo hatari, huku Trump akitaka kufungua nchi ili watu warudi kazini. Vilevile amekuwa akitaka shule zifunguliwe kwa wanafunzi kuendelea mbele na masomo. Lakini Fauci amekuwa akishauri kuwa hatua hizo zinapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kuu, ili kuepusha kusambaa kwa virusi vya corona.

Kwa jumla zaidi ya watu milioni tatu wamethibitishwa kuambukizwa nchini Marekani na zaidi ya watu 137,000 wamefariki tangu janga hilo lilipoanza.

Uhispania, moja ya nchi za Ulaya zilizoathiriwa zaidi na janga hilo, kwa upande wake inatarajia leo Alhamisi kutoa heshima za mwisho kwa waathiriwa wa virusi hivyo, huku ikiendelea kuwa makini kwa kufuatilia kwa karibu zaidi ya familia 120 zilizoambukizwa virusi vya Corona nchini humo.

Kufikia sasa zaidi ya watu milioni 13.4 wameambukizwa virusi vya Corona na karibu vifo 580,000 vimeripotiwa duniani kote.

Duniani kote sasa janga hilo limesababisha nchi mbalimbali kuchukua tena masharti ya raia wao kubaki nyumbani na hatua zingine mpya kama vile uvaaji wa barakoa.