BRAZIL-CORONA-AFYA

Watu karibu 40,000 waambukizwa virusi vya Corona kwa muda wa saa 24 Brazil

Brazil ni nchi iliyoathiriwa zaidi na janga la Covid-19 duniani baada ya Marekani.
Brazil ni nchi iliyoathiriwa zaidi na janga la Covid-19 duniani baada ya Marekani. Amanda Perobelli/Reuters

Brazili imerekodi visa vipya 39,924 vya maambukizi ya Corona yaliyothibitishwa na vifo vipya 1,233 katika muda wa saa 24 zilizopita, Wizara ya Afya imesema katika taarifa.

Matangazo ya kibiashara

Nchi hii ya Amerika Kusini sasa imerekodi jumla ya visa 1,996,748 vya maambukizi ya virusi vya Corona na vifo 75,366 vinavyotokana na ugonjwa huo hatari.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins nchini Marekani, nchi ya Marekani inaongoza kwa maambukizi zaidi ya Milioni tatu na vifo zaidi ya 137,000, ikifutwa na Brazil, India, Urusi na Peru.

Wiki hii Mkurugenzi Mkuu wa shirikja la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus alionya kuwa hali itaendelea kuwa mbaya zaidi iwapo mataifa mbalimbali duniani hayatachukua hatua zaidi za kukabiliana na virusi hivyo.

Janga la corona litakuwa ''baya na baya zaidi'' ikiwa serikali zitashindwa kuchukua hatua madhubuti, Shirika la afya duniani (WHO) lilitahadharisha.

Kufikia sasa zaidi ya watu milioni 13.4 wameambukizwa virusi vya Corona na karibu vifo 580,000 vimeripotiwa duniani kote.

Duniani kote sasa janga hilo limesababisha nchi mbalimbali kuchukua tena masharti ya raia wao kubaki nyumbani na hatua zingine mpya kama vile uvaaji wa barakoa.