BRAZILI-CORONA-AFYA

Idadi ya maambukizi yapindukia Milioni mbili Brazili

Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona nchini Brazil sasa imefikia zaidi ya Milioni Mbili, huku idadi ya vifo ikiongezeka pia na kufikia zaidi ya 76,000.

Brazili yaendelea kukumbwa na Corona.
Brazili yaendelea kukumbwa na Corona. NELSON ALMEIDA / AFP
Matangazo ya kibiashara

Wizara ya afya nchini humo imesema watu wengine zaidi ya 45,000 walipatikana na janga hilo kwa muda wa saa 24 zilizopita, huku watu wengine 1,300 wakipoteza maisha.

Ongezeko hili, linaifanya Brazil kuwa nchi ya pili duniani iliyoathiriwa zaidi na virusi hivi baada ya Marekani ambayo ina visa zaidi ya Milioni tatu na Laki Tano.

Kwa kipindi cha miezi miwili taifa hilo la Amerika Kusini, limekuwa likiripoti maambukizi mapya zaidi ya Elfu 30 kila siku na mara 11 imeripoti visa zaidi ya Elfu 40.

Hata hivyo, kuna wasiwasi kuwa idadi ya watu wanaoripotiwa ni ndogo kwa sababu kuna maeneo ambayo upimaji wa virusi hivyo haufanyiki.

Watalaam wa afya nchini humo wamemlaumu rais Jair Bolsonaro ambaye pia ameambiukizwa virusi vya Corona kwa kushindwa kuja na mpango wa kudhibiti maambukizi hayo.