MAREKANI-MAANDAMANO-USALAMA

Trump atishia kutuma askari kuzima maandamano katika miji mbalimbali

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kutuma vikosi vya  usalama katika majimbo yanayoongozwa na Magavana wa chama pinzani cha Democratic, baada ya kuzuka maandamano katika mji wa Oregon, kulalamikia visa vya ubaguzi wa rangi.

Rais wa Marekani Donald Trump amerejelea wito wa utekelezaji sheria na utaratibu.
Rais wa Marekani Donald Trump amerejelea wito wa utekelezaji sheria na utaratibu. MANDEL NGAN / AFP
Matangazo ya kibiashara

Trump amewashtumu Mameya wa miji inayoongozwa na chama cha Democratic kama New York, Chichago na miji mingine kwa kuwaogopa waandamanaji anaowashtumu kufuja na kuharibu mali ya watu kwa sababu za kisiasa.

Viongozi wa majimbo wamemuomba Rais Trump kuondoa maafisa alioagiza kutumwa huko Portland na kumshutumu kwa kufanya hali kuwa mbaya zaidi kama njia ya kutafuta ushawishi wa kisiasa wakati nchi yake ikijiandalia uchaguzi wa urais mwezi Novemba mwaka huu.

Mji wa Portland umekuwa ukishuhudia maandamano dhidi ya ukatili unaotekelezwa na polisi mjini humo tangu kutokea kwa mauaji ya George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuawa akiwa mikononi mwa polisi huko Minnesota mnamo mwezi Mei mwaka huu.

Maafisa 150 wanatarajiwa kutumwa Chicago wiki hii, ili kusaidia maafisa wengine wa serikali pamoja na maafisa polisi wa Chicago kupambana na uhalifu.