MAREKANI-CORONA-AFYA-SIASA

Marekani: Wabunge watakiwa kuvaa barakoa Marekani

Nancy Pelosi amesema chini ya kanuni hiyo mpya wabunge wataruhusiwa tu kuondoa barakoa wakati wa kuhutubia au kutoa michango mbele ya Bunge.
Nancy Pelosi amesema chini ya kanuni hiyo mpya wabunge wataruhusiwa tu kuondoa barakoa wakati wa kuhutubia au kutoa michango mbele ya Bunge. REUTERS/Erin Scott

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi ametangaza kwamba wabunge na wafanyakazi wote katika Bunge hilo watapaswa kuvaa barakoa kwenye makao makuu ya bunge katika kipindi chote cha janga la virusi vya Corona.

Matangazo ya kibiashara

Wabunge wataruhusiwa kuondoa barakoa wakati wa kuhutubia au kutoa michango mbele ya Bunge, amesema Nancy Pelosi kutoka makao makuu ya Bunge.

Hii inahitajika kama ishara ya "kuheshimu afya, usalama na ustawi wa wengine katika makao makuu ya Bunge na maeneo jirani," Pelosi ameongeza.

Uamuzi huo unakuja baada ya mmoja wa wabunge kutoka chama cha Republican Louie Gohmert, aliyepinga vikali uvaaji wa barakoa tangu kuzuka kwa janga nchini Marekani, kutangaza siku ya Jumatano kwamba alikutwa na virusi vya Corona baada ya kupimwa. Wakati huo huo wenzake watatu walitangaza kwamba wamejiweka karantini.

Hayo yanajiri wakati Marekani imefikisha idadi ya vifo 150,000 vya COVID-19 ambayo ni kubwa kuliko taifa lingine lolote duniani.