MAREKANI-TEUMP-TWITTER-FACEBOOK-CORONA-AFYA

Twitter na Facebook wazuia ujumbe wa Donald Trump kutokana na taarifa potofu za Covid-19

Twitter ni chombo cha habari namba moja cha rais wa Marekani Donald Trump.
Twitter ni chombo cha habari namba moja cha rais wa Marekani Donald Trump. OLIVIER DOULIERY / AFP

Utawala wa mitandao ya kijamii ya Twitter na Facebook ,umefuta chapisho na kanda za video  na kuondoa ukurasa wa rais wa Marekani Donald Trump kwa msingi zilikuwa habari za kupotosha kuhusu Covid-19.

Matangazo ya kibiashara

Kupitia ukurasa wake rais Trump alisema watoto wana kinga tosha dhidi ya Corona ,msimamo ambao ni tofauti na msimamo wa idara ya afya ya nchi hiyo.

Msemaji wa Facebook amesema kuwa ujumbe huo ni wa uongo.

Ujumbe wa Twitter wenye vidio hiyo hiyo ambao awali ulitumwa na timu ya kampeni ya Trump nao pia ulifichwa na Twitter kwa sababu hizo hizo.

Msemaji wa Twitter amesema timu hiyo ya kampeni inapaswa kwanza kuuondowa ujumbe huo kabla hawajaruhusiwa tena kuutumia mtandao huo

Wakati huo huo mtalaam wa magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani Dkt Anthony Fauci amesema kampuni nyingi za kutengeneza dawa ,zitakuwa na mamilioni ya chanjo kufikia mwaka wa 2021.

Fauci amebaini kwamba hii ni kutokana na kampuni hizo kuanza kutengeneza chanjo hizo hata kabla kujaribiwa rasmi na kuthibitishwa zinafanya kazi.

Hayo yanajiri wakati China na Shirika la Afya Duniani, WHO, zinajadili mipango ya kubaini chanzo cha mripuko wa virusi vya corona, kufuatia ziara nchini humo, ya wataalamu wawili wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa.

Virusi vya Corona vilibainika kwa mara ya kwanza katika mji wa Wuhan katikati mwa China, mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, na vimehusishwa na soko la jumla la vyakula, ambako wanyama wa porini wanauzwa.