MAREKANI-CORONA-AFYA

Idadi ya maambukizi yapindukia Milioni 5 nchini Marekani

Nje ya Hospitali ya Elmhurst Hospital Center katika eneo la Queens Borough huko New York City, Marekani Aprili 24, 2020.
Nje ya Hospitali ya Elmhurst Hospital Center katika eneo la Queens Borough huko New York City, Marekani Aprili 24, 2020. REUTERS/Lucas Jackson

Idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona nchini Marekani sasa imefikia zaidi ya Milioni TANO, wakati huu watalaam wa afya wakibashiri kuwa chanjo itapatikana kufikia mwisho wa mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Watalaam wa afya nchini humo wanasema, mtu mmoja kati ya 66 wameambukizwa virusi hivyo, huku idadi ya vifo nayo ikiongezeka na kufikia zaidi ya 160,000.

Marekani inashuhudia ongezeko hilo wakati huu rais Donald Trump akitia saini agizo linalotarajiwa kuwasaidia kiuchumi raia wa nchi hiyo walioathirika pakubwa na janga hili.

Kwingineko, nchini Brazil takwimu za hivi punde zinaonesha kuwa idadi ya vifo imevuka watu Laki Moja, katika kipindi cha miezi mitano, huku watu wengine Milioni Tatu, wakiambukizwa.

Kwingineko duniani, New Zealand imemaliza siku 100 bila ya maambukizi mapya lakini inaonya kuwa kuongezeka kwa nchi jirani kama Vietnam na Australia huenda hali hiyo ikatishia nchi yake.

Duniani, watu Milioni 19.5 wameambukizwa na virusi vya Covid 19, wengine zaidi ya Milioni 11 wamepona, huku idadi ya vifo ikiongezeka na kufikia zaidi ya 725,000.