MAREKANI-TRUMP-SIASA

Marekani: Mshauri wa karibu wa Trump, Kellyanne Conway ajiuzulu

Mshauri wa karibu wa Donald Trump, Kellyanne Conway ajiuzulu na kusema kuwa anakwenda kuwa karibu na familia yake.
Mshauri wa karibu wa Donald Trump, Kellyanne Conway ajiuzulu na kusema kuwa anakwenda kuwa karibu na familia yake. JIM WATSON / AFP

Kellyanne Conway, mshauri wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump anayejulikana kwa maneno yake makali dhidi ya waandishi wa habari, ametangaza kwamba anajiuzuli na amesema anataka kukaa karibu na familia yake.

Matangazo ya kibiashara

Mshauri huyo katika masuala ya mawasiliano, mwenye umri wa miaka 53, amekuwa karibu na Donald Trump tangu siku ya kwanza, akiongoza kampeni ya uchaguzi mwaka 2016 ambayo ilimpelekea Donald Trump kushinda uchaguzi wa urais.

Lakini miaka yote minne imemalizika Kellyanne Conway akimtetea rais wa Marekani, hasa kwenye runinga.

Wengi wamekuwa wakijiuliza kuhusu mwanamke huyu, wakati mumewe ambaye ni wakili wa kihafidhina George Conway, ni mmoja wa wakosoaji wa Donald Trump, ambaye amekuwa akihoji kuhusu uwezo wake wa kiakili kwa kuongoza nchi.

Katika taarifa, Kellyanne Conway ametangaza kwamba ataondoka White House "mwishoni mwa mwezi huu".

Uamuzi huu "ni chaguo langu kabisa", amesema, na kuongeza kuwa atatangaza "mipango yake ya baadaye katika muda muafaka". "George pia anafanya mabadiliko kadhaa. Sikubaliani nae kwa mambo mengi, lakini tumeungana kwa mambo muhimu zaidi: watoto, "ameongeza.

Hayo yanajiri wakati Dada wa rais wa Marekani Donald Trump amemuelezea rais huyo kama mkatili na muongo na asiyepaswa kuaminiwa, hii ikiwa ni kwa mujibu wa sauti yake iliyorekodiwa kisiri na kuchapishwa Jumamosi Agosti 22.

Rekodi hizo kwa mara ya kwanza ziliripotiwa na gazeti la The Washington Post, ambapo baadae shirika la habari la AP lilizipata.

Kauli hiyo ya kukosoa iliyotolewa na Maryanne Trump Barry ilirekodiwa na mpwa wake, Mary Trump, ambaye mwezi uliopita alichapa kitabu kilichomkosoa rais huyo.