MAREKANI-KENOSHA-MAANDAMANO-USALAMA

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi yaendelea kabla ya ziara ya Trump Kenosha

Maafisa wa polisi watawanya umati wa waandamanaji huko Portland mnamo Agosti 29, 2020.
Maafisa wa polisi watawanya umati wa waandamanaji huko Portland mnamo Agosti 29, 2020. Nathan Howard/Getty Images/AFP

Maandamano dhidi ya vitendo viovu vya polisi yanaendelea nchini Marekani katika miji ya Kenosha na Portland ambapo mtu mmoja aliuawa katika makabiliano kati ya waandamanaji wa vuguvugu la Black Lives Matter na wafuasi wa Donald Trump.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Marekani anaendelea kuwataka raia kuheshimu sheria na na amewashutumu maafisa wa miji hiyo kwa kuruhusu machafuko.

Donald Trump amethibitisha kwamba miezi ya mwisho ya kampeni yake itaelekezwa kwa kile anachokiita "sheria na utaratibu" dhidi ya maandamano ya sasa.

Donald Trump pia ametoa rambi rambi zake kwa familia ya mtu aliyepigwa risasi na kuuawa huko Portland Jumamosi wakati wa makabiliano kati ya wafuasi wake na waandamanaji kutoka vuguvugu la Black Lives Matter.

Wakati huo huo rais wa Marekani Donald Trump na mpinzani wake wa Democratic Joe Biden wameshutumiana kutokana na vurugu zilizotokea huko Portland, Oregon.

Portland imekuwa kitovu cha maandamano dhidi ya ukatili unaotekelezwa na polisi na ubaguzi wa rangi tangu kutokea kwa mauaji ya George Floyd, Mmarekani mweusi huko Minneapolis, Mei 25 na kusababisha ghadhabu nchini na hata kimataifa.

Hayo yanajiri wakati rais wa Marekani Donald Trump anatarajia kuzuru mji wa Kenosha, katika Jimbo la Wisconsin, Jumanne wiki hii, eneo ambapo Mmarekani mweusi Jacob Blake alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na afisa wa polisi, kesi ambayo imezusha maandamano makubwa nchini Marekani dhidi ya ubaguzi wa rangi.