VENEZUELA-HAKi-SIASA-USALAMA

Venezuela yawasamehe wapinzani wengi kabla ya uchaguzi wa wabunge

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, ambaye uhalali wake unapingwa na ipinzani na nchi kadhaa za Magharibi.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, ambaye uhalali wake unapingwa na ipinzani na nchi kadhaa za Magharibi. REUTERS/Manaure Quintero

Venezuela imetangaza kuwa imewasamehe zaidi ya wanasiasa wa upinzani 100, wakiwemo wabunge zaidi ya 20 ambao walituhumiwa kupanga njama dhidi ya rais Nicolas Maduro, wakati uchaguzi wa wabunge utafanyika katika nchi hii ya Amerika Kusini mwezi Desemba.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hii inaonyesha kwamba chama cha Kisoshalisti kilicho madarakani kinakusudia kukuza ushiriki katika uchaguzi huo, baada ya sehemu ya upinzani kutangaza kwamba wataususia kutokana na udanganyifu.

Miongoni mwa wanasiasa waliosamehewa na agizo la rais ni pamoja na mbunge Freddy Guevara, ambaye alikuwa ameomba hifadhi katika ubalozi wa Chile, na Roberto Marrero, ambaye alikuwa katibu mkuu wa kiongozi wa upinzani na spika wa Bunge, Juan Guaido.

"Tuna imani kuwa hatua hizi (...) zitasaidia kudumisha mwelekeo wa kidemokrasia kwa wanasiasa wote", ametangaza Waziri wa Habari, Jorge Rodriguez, wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Majina mengi yaliyotajwa yalishiriki katika maandamano yaliyozimwa mwaka jana yaliyolenga kushawishi jeshi kumtimuwa rais Nicolas Maduro, ambaye uhalali wake unapingwa na upinzani na nchi nyingi.

Baadhi ya wanasiasa hao walikuwa wamezuiliwa jela, wakati wengine wameomba hifadhi ya kisiasa na wengine wako uhamishoni.

"Maduro sio rais na mimi sio mhalifu," amejibu mbunge Americo de Grazia, ambaye jina lake liko kwenye agizo la rais la wabunge waliopewa msamaha. "Ikiwa unataka kusaidia kupatikana kwa amani, omba msamaha kwa wananchi wa Venezuela kwa kushikilia madaraka kinyume cha sheria, " ameongeza mbunge Americo de Grazia.

Agizo hilo halimtaji Leopoldo Lopez, mmoja wa vigogo wa upinzani, ambaye alifungwa mwaka 2014 kwa kuongoza maandamano dhidi ya rais Nicolas Maduro na sasa anaishi katika ubalozi wa Uhispania.