MAREKANI-USALAMA

Marekani: Los Angeles yakumbwa na maandamano baada ya kifo cha mtu mweusi aliyeuawa na polisi

Waandamanaji walikusanyika huko Los Angeles kupinga kifo cha Dijon Kizzee, Mmarekani mweusi aliyeuawa na polisi Agosti 31, 2020.
Waandamanaji walikusanyika huko Los Angeles kupinga kifo cha Dijon Kizzee, Mmarekani mweusi aliyeuawa na polisi Agosti 31, 2020. REUTERS/Patrick T. Fallon

Raia wenye hasira wameendelea na maandamano katika mji wa Los Angeles wakidai majibu baada ya kifo cha mtu mweusi aliyeuawa Jumatatu na polisi, ambayo inadai kuwa alikuwa na silaha ndogo aina ya bastola, katika hali ya mvutano mpya iliyozushwa na kisa cha Jacob Blake.

Matangazo ya kibiashara

Umati mdogo wa watu walikusanyika Jumanne jioni katika eneo la tukio na kisha waliandamana kwa amani, wakiongozana na msafara wa magari, hadi kituo cha polisi. Baadhi ya waandamanaji walikuwa wamebebelea mabango yaliyoandikwa "Tunalaani polisi inayojihusisha na mauaji".

Kulingana na vyombo vya habari nchini Marekani, karibu watu 100 walikuwa wamekusanyika eneo la tukio Jumatatu jioni, wakati kulikuwa kukifanyika maandamano mengine ya kupinga ubaguzi wa rangi yaliyozuka nchini Marekani baada ya afisa wa polisi, mzungu, kumpiga risasi saba mtu mweusi huko Kenosha, katika Jimbo la Wisconsin.

Mhanga, aliyetambulika kama Dijon Kizzee, 29, alikuwa akiendesha baiskeli Jumatatu alasiri katika kitongoji cha kusini mwa Los Angeles wakati maafisa wa eneo hilo walijaribu kumzuia kwa ukiukaji wa sheria za barabarani. Idara ya usalama ya Los Angeles hazijaainisha kwa sasa ni kosa gani alishtumiwa kufanya.

'Polisi walimpiga risasi zaidi ya 20 mgongoni'

Kulingana na maelezo ya mamlaka, Dijon Kizzee "aliondoka mbio" baada ya kuacha baiskeli yake. Polisi walifanikiwa kumkamata. Ni wakati huu, Luteni Brandon Dean aliwaambia waandishi wa habari, kwamba kijana huyo Mmarekani mweusi "alimpiga mmoja wa maafisa usoni."

Mshukiwa aliangusha rundo la nguo alizokuwa amebebelea mkononi mwake. "Maafisa waligundua kuwa bastola nyeusi ilikuwa ndani ya rundo la nguo," afisa huyo ameongeza. kisha maafisa wa polisi wakafyatua risasi. Mtu huyo, aliyepigwa na risasi kadhaa, alifariki dunia papo hapo.

Wakili Ben Crump, ambaye anawakilisha familia ya Dijon Kizzee, amewataka mashahidi kuwasiliana naye. "Wanasema alikimbia, akaacha nguo na bunduki," Ben Crump ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake aw Twitter. “Hakuichukua, lakini polisi walimpiga risasi zaidi ya 20 mgomgoni mwake na kisha kumuacha hapo kwa saa kadhaa. "