VENEZUELA-EU-UN-UCHAGUZI-USHIRIKIANO

Venezuela: Maduro aalika EU na UN kutuma waangalizi kwenye uchaguzi wa wabunge

Rais wa venezuela, Nicolas Maduro.
Rais wa venezuela, Nicolas Maduro. REUTERS/Fausto Torrealba

Serikali ya Venezuela imetangaza kuwa imealika Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya (EU) kutuma waangalizi wa uchaguzi wa wabunge uliopangwa kufanyika Desemba 6.

Matangazo ya kibiashara

"Ninawaarifu kuwa siku ya Jumanne tulimtumia barua Antonio Guterres na Josep Borrell kuhusu kufanyika kwa uchaguzi ujao wa wabunge, (...) na tumetoa mwaliko kwa Umoja wa Mataifa na Umoja Umoja wa Ulaya kutuma waangalizi wao, " Waziri wa Mambo ya nje wa Venezuela Jorge Arreaza ameandika kwenye Twitter.

Barua hii, ambayo baadaye ilirushwa kwenye mtangao wa Twitter, inapendekeza "mfumo wa dhamana" unaotokana na "mchakato mkubwa wa mazungumzo", ikiwa ni pamoja na "marekebisho" kwenye kalenda ya uchaguzi ili kukuza ushiriki na kuongeza wino usiyofutika ambamo wapiga kura watapaswa kutumbukiza vidole vyao baada ya kupiga kura, mfumo ulifutwa katika uchaguzi wa urais uliozua utata wa mwaka 2018, wakati rais Nicolas Maduro alipochaguliwa kwa muhula mwingine.

"Tunayo furaha ya kukualikeni kama wangalizi na wasaidizi wa kimataifa katika uchaguzi huu, na tunahakikisha kwamba majukumu mliyopewa yatazingatiwa kama sehemu ya hatua zinazolenga kuhakikisha uaminifu katika uchaguzi huu", barua hiyo imeongeza.

Mwaliko huu unakuja siku moja baada ya msamaha uliotolewa na Nicolas Maduro kwa wapinzani zaidi ya 100, wakiwemo wabunge na wasaidizi wa kiongozi wa upinzani Juan Guaido, ili "kuendeleza maridhiano ya kitaifa", miezi mitatu kabla ya uchaguzi huu wa wabunge ambao upinzani unatoa wito wa kususia.