MAREKANI-CORONA-AFYA

Coronavirus / Marekani: Trump apingana na mkuu wa CDC kuhusu chanjo

Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa mkutano na waandishi wa habari, ikulu ya White House.
Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa mkutano na waandishi wa habari, ikulu ya White House. REUTERS/Leah Millis

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba angalau dawa milioni 100 ya chanjo dhidi ya Corona zinaweza kusambazwa nchini Marekani ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, akipingana na kauli ya mkurugenzi wa Vituo vya kuzuia na Kudhibiti magonjwa nchini humo (CDC).

Matangazo ya kibiashara

Mapema Jana mchana, Robert Redfield alisema kuwa chanjo ya ijayo ya Corona inaweza kutolewa kwa idadi kubwa katikati ya mwaka wa 2021 au mapema kidogo.

"Alifanya makosa aliposema hivyo," amebaini Donald Trump, na kuongeza mbele ya waandishi wa habari kwamba alizungumza kwa simu na Robert Redfield. "Nadhani alikuwa amechanganyikiwa. Labda hakuelewa swali hilo," ameongeza rais wa Marekani, ambaye hivi karibuni aliidhinishwa na chama chake cha Republican kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa urais ambao umepangwa kufanyika Novzmba 3.

Huku mamilioni ya watu wakiwa bado wanakabiliwa na athari za maambukizi ya Corona na ugonjwa wa COVID -19, mbio za kutafuta chanjo ulimwenguni kote zinaendelea. Kampuni tisa tayari zikiwa katika awamu ya tatu ya majaribio ya chanjo ya Corona.

Kampuni ya AstraZeneca imesema ina matumaini kwamba chanjo inaweza kupatikana hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao. Chuo Kikuu cha Oxford kimesema katika majaribio makubwa kama haya, inatarajiwa kwamba baadhi ya washiriki watakuwa wagonjwa na kwamba kila tukio lazima lichunguzwe kwa uangalifu.