MAREKANI-TRUMP-UCHAGUZI-SIASA

Trump hajakuwa tayari kukabidhi madaraka kwa amani

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipoulizwa iwapo atakubali kushindwa na kukabidhi madaraka, rais Donald Trump alisikika akisema wataangalia kile kitakachojitokeza.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipoulizwa iwapo atakubali kushindwa na kukabidhi madaraka, rais Donald Trump alisikika akisema wataangalia kile kitakachojitokeza. REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump, amekataa kuweka wazi iwapo atakabidhi madaraka kwa amani iwapo atapoteza Uchaguzi wa urais utakaofanyika mwezi Novemba.

Matangazo ya kibiashara

Trump, anapambana na Joe Biden kutoka chama cha Democratic katika uchaguzi ambao wachambuzi wa siasa wanasema ni kipimo cha utendakazi wake kwa miaka minne aliyokuwa madarakani.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, alipoulizwa iwapo atakubali kushindwa na kukabidhi madaraka, rais Trump alisikika akisema wataangalia kile kitakachojitokeza.

“Mara kadhaa nimekuwa nikilalamikia mchakato wa upigaji kura na kwamba hali hiyo ni janga.

Kwa takribani mwezi sasa kiongozi huyo ambae anawania muhula wa pili madarakani, amekuwa katika kampeni dhidi ya upigaji kura kwa njia ya barua katika uchaguzi wa Marekani kwa kutumia ukurasa wake wa Twitter na kukosoa wazi kuhusu utaratibu huo.

Mwaka 2016, rais Donald Trump alikataa kujitolea kukubali matokeo ya uchaguzi katika kinyang'anyiro kati yake na mgombea wa Democratic , Hillary Clinton, hatua ambayo alitaja kama shambulio dhidi ya demokrasia ya Marekani.

Hata hivyo alitangazwa kuwa mshindi, licha ya kuwa hakupata kura za wengi ambazo pia bado anatilia shaka.