USA 2020: Sheria mpya kuchukuliwa kwa midahalo kabla ya uchaguzi Marekani
Imechapishwa:
Kundi linaloandaa na kusimamia mijadala ya wagombea urais nchini Marekani imesema kwamba itachukua hatua kuhakikisha midahalo mikubwa miwili inayofuata, kati ya Donald Trump na Joe Biden, ifanyike katika mazingira bora.
Hatua hiyo inakuja baada ya mdahalo wa kwanza wa moja kwa moja kwa njia ya televisheni kati ya wagombea wakuu wa uchaguzi wa Novemba 3 nchini Marekani, Donald Trump na Joe Biden, kugeuka kuwa uwanja wa shutuma, tuhuma na kufokeana.
Tume ya Mijadala ya wagombea urais, kundi lisiloegemea upande wowote linaloandaa na kusimamia midahalo hii tangu 1988, limesema litabadilisha muundo wa mijadala ili kuepusha uhasama, bila hata hivyo kutoa maelezo ya hatua zitakazochukuliwa.
"Mjadala wa Jumanne usiku ulionesha kuwa kuna haja ya sheria zihusuzo mijadala inayosalia ili kuhakikisha midahalo hiyo inafanyika katika mazingira bora na kila mmoja kujibu vilivyo maswali yanyoulizwa," kundi hilo limesema katika taarifa.
Donald Trump na Joe Biden watapambana tena Oktoba 15 na 22 kwa ajili ya uchaguzi wa urais wa Novemba 3.