MAREKANI-CORONA-UCHUMI

Trump asitisha mazungumzo juu ya mpango wa msaada wa uchumi wa Marekani

Rais Donald Trump akiondoka Hospitali ya Walter-Reed alikokuwa akitibiwa Covid-19, Oktoba 5, 2020.
Rais Donald Trump akiondoka Hospitali ya Walter-Reed alikokuwa akitibiwa Covid-19, Oktoba 5, 2020. REUTERS/Jonathan Ernst

Rais wa Marekani Donald Trump, amesitisha mazungumzo yanayoendelea kuhusu mswada wa kusaidia watu walioathrika na virusi vya Corona na kusema watalipwa fedha na serikali hadi uchaguzi mkuu utakapomaliza mwezi Novemba.

Matangazo ya kibiashara

Mpinzani wake Joe Biden ameshtumu uamuzi huu wa Trump na kusema ameamua kuwageuzia mgongo raia wa Marekani.

Mazungumzo kuhusu mswada huo yamekuwa yakiendelea kati ya spika wa bunge Nancy Pelosi na Waziri wa fedha Steven Mnuchin tangu mwezi Julai.

Agizo hilo la ghafla la mazungumzo ya muda mrefu juu ya kifurushi kipya cha bajeti limekosolewa na Joe Biden, wabunge na maseneta kutoka chama cha Democratic lakini pia na baadhi ya wabunge na maseneta wa chama cha Republican, wakibaini kwamba kuna ulazima wa kutoa msaada wa ziada kwa mamilioni ya Wamarekani ambao wamepoteza kazi zao tangu kuzuka kwa mgogoro wa kiafya unaoyosababishwa na virusi vya Corona.

Marekani ni nchi iliyoathirika zaidi duniani na janga COVID-19, ikiwa na zaidi ya wagonjwa milioni 7 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya Corona na zaidi ya vifo 210,000.

Hili ni tangazo kubwa la kwanza la Donald Trump tangu arudi White House Jumatatu jioni, hata wakati idadi ya visa vipya vya maambukizi vikiongezeka katika sehemu kubwa ya nchi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi kutoka chama cha Democratic, alibaini kwenye runinga ya NBC siku ya Jumapili kuna hatua ambayo imepigwa katika mazungumzo hayo.

"Rais amewageuzia kisogo," Joe Biden ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, akiujibu uamuzi wa rais anayemaliza muda wake wa kusitisha mazungumzo hadi uchaguzi wa Novemba 3.