BOLIVIA-UCHAGUZI-SIASA

Uchaguzi wa urais kufanyika Bolivia, mwaka mmoja baada ya Morales kujiuzulu

Maandalizi ya vifaa vya uchaguzi huko La Paz, Oktoba 16, 2020
Maandalizi ya vifaa vya uchaguzi huko La Paz, Oktoba 16, 2020 AFP

Karibu mwaka mmoja baada ya kujiuzulu kwa kiongozi wa zamani wa Kisoshalisti Evo Morales, raia wa Bolivia wanapiga kura leo Jumapili kumchagua rais wao mpya katika nchi ambayo imegawanyika, ambapo wito emeendelea kutolewa ili kuepusha mgogoro mpya wa kisiasa.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mara ya kwanza katika miaka 20, Evo Morales (2006-2019), kiongozi wa kihistoria wa mrengo wa kushoto katika kanda ya Amerika Kusini, sio mgombea katika uchaguzi huo.

Novemba 10, 2019, alijiuzulu baada ya Bolivia kutumbukia katika mzozo wa kisiasa, akituhumiwa na upinzani wizi wa kura, wakati alikuwa akiwania muhula wa nne.

Waziri wake wa zamani wa Uchumi, Luis Arce, 57, mgombea kutoka chama cha MAS, na mpinzani wake mkuu, rais wa zamani Carlos Mesa, 67, ndio wanapewa nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huu ambao wanachuana wagombea sita.

Kulingana na uchunguzi, Bwana Arce, anayechukuliwa kama baba wa "muujiza wa (uchumi) wa Bolivia, anaongoza kwa kura katika duru ya kwanza, lakini hatoipuka duru ya pili, iliyopangwa Novemba 29.

Wabolivia milioni 7.3 wanapiga kura kumchagua rais wao, lakini pia makamu wao wa rais, na kuwachagua wabunge wapya, bunge ambalo kwa sasa linatawaliwa na chama cha MAS. Kutokana na janga la Corona, kampeni ya uchaguzi ilifanyika kupitia mitandao ya kijamii.Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 2 asubuhi na zitafungwa saa 11 jioni saa za Bolivia.

Mahakama ya Uchaguzi ilisema Jumamosi kuwa, ili kuepusha mvutano matokeo ya awali hayatatangazwa: "hatutakuwa na matokeo rasmi na ya mwisho Jumapili jioni. Tutajipa muda zaidi, na ni muhimu kwamba raia waonyeshe uvumilivu kwa sababu matokeo yatakuwa ya kuaminika, "amesema Mkuu wa mahakama inayoshughulikia masuala ya uchaguzi, Salvador Romero.