MAREKANI-UCHAGUZI-SIASA

USA 2020: Trump kufanya kampeni Arizona, Biden kuzungumzia kuhusu COVID-19

Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa mdahalo wa pili na wa mwisho na Joe Biden kabla ya uchaguzi wa urais, Oktoba 22, 2020 huko Nashville.
Rais wa Marekani Donald Trump wakati wa mdahalo wa pili na wa mwisho na Joe Biden kabla ya uchaguzi wa urais, Oktoba 22, 2020 huko Nashville. AP Photo/Julio Cortez

Donald Trump anatarajia kufanya mikutano miwili leo Jumatano huko Arizona, jimbo muhimu kwa uchaguzi wa urais Jumanne ijayo nchini Marekani ambapo uchunguzi unamuonyesha akiwa nyuma ya mpinzani wake kutoka chama cha Democratic Joe Biden.

Matangazo ya kibiashara

Joe Biden, ambaye anaendelea kumkosoa rais anayemaliza muda wake kwa usimamizi wake katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19, kwa upande wake atawapokea wataalam wa afya ya umma na atatoa hotuba huko Delaware hukusu mipango yake ya kupambana na COVID-19, timu yake ya kampeni imebaini.

Zaidi ya Wamarekani milioni 70 tayari wamepiga kura ya mapema, kulingana na takwimu kutoka US Elections Project.

Kwa sababu ya idadi kubwa ya kura kwa njia ya posta, zoezi la uhesabuji kura linaweza kuchukua siku kadhaa au hata wiki kadhaa, wataalam wanasema, na jina la mshindi wa uchaguzi halitaweza kujulikana Novemba 3.

"Ingelikuwa sahihi na vizuri sana ikiwa mshindi angelitangazwa Novemba 3 badala ya kuhesabu kura kwa wiki mbili, muda ambao haufai kabisa na ambao sidhani hata ikiwa ni kwa mujibu wa sheria zetu," Donald amesema mbele ya waandishi wa habari.

Rais wa Marekani atafanya kampeni yake kwenye uwanja wa ndege wa Bullhead City kaskazini mwa jimbo la Arizona kabla ya kuelekea Goodyear, karibu na Phoenix, jiji kubwa zaidi la jimbo hilo.

Arizona ni moja ya majimbo muhimu katika kinyang'anyiro cha urais na uchunguzi wa Reuters / Ipsos unampa Joe Biden alama tatu mbele ya Donald Trump.