MAREKANI-UCHAGUZI-SIASA-USALAMA

Wamarekani kumchagua rais wao mpya Jumanne hii

Wananchi wa Marekani wanapiga kura leo Jumanne kumchagua rais wao mpya kati ya wagombea wawili Donald Trump wa chama cha Republican na Joe Biden kutoka chama cha Democratic.

Joe Biden na Donald Trump.
Joe Biden na Donald Trump. AP/Patrick Semansky
Matangazo ya kibiashara

Kulingana na kura za maoni ya umma, kufikia Jumatatu wiki hii, Joe Biden alikuwa anaongoza dhidi ya Donald Trump.

Saa chache kabla ya kufunguliwa vituo vya kupigia kura katika siku ya uchaguzi wa Marekani unaofanyika leo, rais Donald Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic walitumia siku nzima ya Jumatatu kuwashawishi wapiga kura kuwapatia ushindi.

Trump ambaye amekuwa rais kwa miaka minne iliyopita hakuwahi hapo kabla kushika nafasi ya uongozi na anajaribu kujitofautisha na Biden, seneta na makamu wa rais wa zamani ambaye amekuwepo kaitka siasa za Marekani kwa miongo minne iliyopita.

Naye Biden aliyeongozana na wajukuu zake wanne kwenye mkutano mjini Ohio amesema Trump amegeuka na kuwa kituko mbele ya viongozi wengine wa dunia.

Hadi kufikia sasa wamarekani milioni 97 kati ya milioni 225 wenye sifa ya kupiga kura tayari wameshiriki upigaji kura wa mapema na kuweka rekodi ya kuwa idadi kubwa kabisa ya watu kujitokeza kushiriki uchaguzi kabla ya kilele ambayo ni siku ya uchaguzi.