UCHAGUZI MAREKANI 2020

Trump adai kuibiwa kura, Biden ajipa imani kushinda

Rais wa Marekani, Donald Trump, ameendelea kuibua mjadala zaidi nchini humo baada ya kuandika kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, kuna wizi mkubwa unaofanyika wakati hesabu za kura zikiendelea.

Donald Trump, akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni hivi karibuni, 24 octobre 2020.
Donald Trump, akiwa katika moja ya mikutano yake ya kampeni hivi karibuni, 24 octobre 2020. REUTERS/Tom Brenner
Matangazo ya kibiashara

Katika kile kinachoonekana ni kujaribu kutengeneza sintofahamu zaidi katika uchaguzi ambao tayari umewagawa Wamarekani, rais Trump, anazidisha joto zaidi baada ya kudai kuwa anaibiwa kura.

Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa twitter, rais Trump, ameandika "Tunashinda pakubwa, wanajaribu kuiba kura, na kamwe hatuwezi ruhusu hilo litokee", aliandika rais Trump.

Matamshi yake tayari yameamsha hisia zaidi nchini humo, huku akiongeza hofu ya kutokea vurugu ikiwa atashindwa katika uchaguzi huu.

Ikumbukwe kuwa tayari alishatangaza tangu awali kuwa huenda asikubaliane na matokeo ya uchaguzi huu aliodai kuna njama za kumuibia kura.

Kwa upande wa mpinzani wake Joe Biden, yeye amejitokeza na kudai kuwa wana imani ya kuibuka na ushindi na kwamba anatambua huenda matokeo yakachukua muda kutangazwam akiwataka raia wa nchi hiyo kuwa watulivu.

Licha ya kutodai moja kwa moja kuwa ataibuka na ushindi, badala yake Biden, amewatia moyo wafuasi wake akisema anafahamu uchaguzi huu ungekuwa wa ushindani na mwisho wa siku "Wananchi ndio watakaoamua" alisema Biden.